SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA VIONGOZI WA DINI - MAJALIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 7, 2025

SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA VIONGOZI WA DINI - MAJALIWA




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inawaamini na inathamini mchango wa viongozi wa dini wa madhehebu yote.

Amesema serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na viongozi hao ili kujenga amani, mshikamano na ustawi wa jamii ya watanzania.

"Tunaamini mtaendeleza jukumu la kuwasihi watanzania waone umuhimu wa kila mmoja kuwa sehemu ya mchango wa kulifanya taifa hili kuwa tulivu na kuimarisha mshikamano miongoni mwetu."

Ameyasema hayo leo (Jumamosi Juni 7, 2025) alipokuwa mgeni rasmi katika Sala na Baraza la Eid Al Adha iliyofanyika katika Msikiti wa Mohamed VI Kinondoni, Dar es Salaam.

Amesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuwajenga waumini wao kuwa na staha, ustaarabu, uvumilivu na kutambua kuwa wao ni miongoni mwa wanajamii na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo.

"Kwa upande wa serikali tunaendelea kujenga misingi ya mshikamano kati ya waumini wa dhehebu moja na dhehebu jingine, tukiwa tunaamini kuwa dini zimeendelea kuifanya nchi hii kuwa nchi ya amani wakati wote."

Kadhalika ametoa wito kwa watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini ili nchi iendelee kupata ustawi.

Amesema ni vyema kuwa na uwezo wa kukemea vitendo vyovyote ambavyo vinaashiria kutishia amani nchini.

Aidha, amewasihi watanzania kuendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampe nguvu na afya ya kuendelea kuliongoza taifa hili.

Kadhalika, amewapongeza waislamu waliofanikiwa kutimiza ibada ya Hijja huku akitoa wito kwa waislamu waliopo nchini kuendelea kuwaombea warudi salama.

"Tuendelee kuwaombea wenzetu wakamirishe ibada hiyo, kwetu sisi ni baraka kwa sababu hata sisi wanatuombea."

Pia amewapongeza viongozi wa dini kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana wadogo ili wakue kwa kuzingatia misingi imara ya kuendeleza dini na maadili yake.

"Dini zina ujenzi mkubwa kwa muumini kiimani na tunapowajenga waumini wetu kiimani tuwaingizie imani yenye manufaa kwa taifa".

Naye, Kaimu Mufti wa Tanzania Sheikh Ali Khamis Ngeruko, ametoa wito kwa watanzania kuwa makini wakati wa uchaguzi ili wachague viongozi wenye weledi kwa kumpima namna anavyo wasilisha sera zake.

"Dunia imekuwa na changamoto kubwa ya watu wenye afya ya akili hivyo tunapo wachagua viongozi tuwachague watu ambao afya zao za akili ziko kwenye kiwango cha juu na kinachoridhisha."

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Alhaj Nuru Mruma, amesema Baraza hilo linawahimiza watanzania kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini ili kutoa nafasi kwa shughuli za kimaendeleo kufanyika.

"Baraza linatoa wito kwa kila Mtanzania kwa nafasi yake kulinda na kudumisha amani, kwani bila amani hakutakuwa na maendeleo yoyote katika jamii".





No comments:

Post a Comment