
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ameongoza mamia ya waombolezaji, katika utoaji wa heshima za mwisho na hatimae mazishi ya Mzee Silvin Ibengwe Emmanuel Mongella, mwenza wa mmoja wa viongozi waandamizi wastaafu nchini, Bi. Getrude Mongella, leo Jumamosi tarehe 7 Juni 2025, katika Kijiji cha Kabusungu, Ilemela, mkoani Mwanza.
Shughuli hiyo ya mazishi ya Mzee Mongella, ambaye pia ni baba mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Ndugu John Mongella, ilitanguliwa na ibada ya misa takatifu iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, ikiongozwa na Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, huku mahubiri yakitolewa na Padri George Nzungu.
Mbali ya Balozi Dkt. Nchimbi, viongozi wengine waliojumuika pamoja na waombolezaji katika mazishi hayo ni pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Jumuiya ya Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, mawaziri, viongozi waandamizi wa Chama na Serikali, wabunge na viongozi wa kiroho kutoka madhehebu ya dini mbalimbali nchini.












No comments:
Post a Comment