TAASISI za Umma Nchini zimeagizwa kuweka vipaumbele kwenye mafunzo ya maadili na uwajibikaji kwa viongozi ili kuimarisha uadilifu na utawala bora mahali pa kazi.
Agizo hilo limetolewa jana Jijini Arusha na Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimali Watu, Mosses Pesha kwaniaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tatu ya maadili kwa viongozi wa umma yaliyotolewa na Chuo cha Uhasibu Arusha(IAA) pamoja na Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma.
Pesha alisema serikali imedhamiria kuhakikisha maadili ya utumishi wa umma yanazingatiwa ikiwemo suala zima la uwajibikaji na uadilifu mahali pa kazi na kutoa rai kwa taasisi za umma kuweka kipaumbele zaidi katika mafunzo ili kuhakikisha ufanisi wenye tija kazini unakuwepo ikiwemo uwajibikaji wa viongozi wa umma unakuwa zaidi.
"Endapo mafunzo haya mliyopata mkiyafanyia kazi tutaona tija kwa wakuu wa taasisi, menejimenti na makatibu tawala kwani maadili ni msingi mkubwa katika utumishi wa umma pamoja na uwajibikaji "
Naye Mkuu wa Kitengo cha Utawala na Usalama kutoka chuo cha IAA Dk, Adonijah Abayo akiongea kwaniaba ya Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka alisema chuo hicho kwakushirikiana na Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma wameshirikiana kwa pamoja kutoa mafunzo hayo hususan katika utawala bora ili kuwezesha wakuu wa taasisi, wenyeviti wa bodi zaidi taasisi, wakurugenzi watendaji na makatibu tawala kutoka mikoa mbalimbali wanajengewa uwezo ili kuhakikisha wanaleta tija kazini pia kuendana na kasi ya mabadililo ya teknolojia yanayokua kwa kasi
"Mafunzo haya yanalengo la kukuza utawala bora, ushirikishwaji wa Umma kujenga na kukuza utawala bora ikiwemo ulinzi wa taarifa muhimu"
Huku, Kiongozi wa timu ya wawezeshaji, Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa viongozi hao na anaamini kuona mabadiliko katika ufanisi kazini
Wakati huo huo, mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo Neema Lupembe alishukuru kwa mafunzo hayo ambayo yatakuwa chachu ya ufanisi kazini pamoja na kupata mbinu za kukabiliana na teknolojia inayokuwa kwa kasi sanjari na thamani halisi ya fedha kuonekana kutokana na mbinu walizopata.
No comments:
Post a Comment