MCHENGERWA ATOA TAMKO LA KUVUNJWA KWA MABARAZA NA MIKUTANO YA KAMATI ZA KUDUMU ZA HALMASHAURI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, June 15, 2025

MCHENGERWA ATOA TAMKO LA KUVUNJWA KWA MABARAZA NA MIKUTANO YA KAMATI ZA KUDUMU ZA HALMASHAURI




Na Okuly JULIUS DODOMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ametangaza rasmi tarehe ya kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini, ikiwa ni hatua ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akitoa Tamko hilo leo Juni 15,2025 jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, kifungu cha 84A, na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 178A, amesaini notisi mbili muhimu za kuvunjwa kwa Mabaraza hayo.

"Notisi ya Kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Wilaya, 2025, na ya pili ni Notisi ya Kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Miji, 2025,"

Mchengerwa amesema kuwa, Notisi hizo zinatarajiwa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali hivi karibuni, na zinabainisha kuwa vikao vyote vya Halmashauri pamoja na Kamati zake lazima vikome kufikia tarehe 20 Juni, 2025 — siku saba kabla ya kuvunjwa rasmi kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linatarajiwa kuvunjwa tarehe 27 Juni, 2025.

“Kufanyika kwa kikao chochote cha Halmashauri au Kamati zake baada ya tarehe 20 Juni ni kinyume cha Sheria na Notisi hizi, na Mtendaji Mkuu wa Halmashauri (Mkurugenzi) atawajibika moja kwa moja kwa ukiukwaji huo,” amesema Waziri huyo

Amesema katika kipindi cha mpito baada ya kuvunjwa kwa Mabaraza hayo, Waziri huyo ameeleza kuwa shughuli zote za kiutendaji zitasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, akisaidiwa na Wakuu wa Idara kama wajumbe wa Kamati ya Menejimenti.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa katika kipindi hicho:, hakutakuwa na uanzishaji wa miradi mipya au uwekezaji wowote mpya, haitaruhusiwa kubadili wala kurekebisha miradi, maamuzi au uwekezaji uliopitishwa kabla ya kuvunjwa kwa Mabaraza.

"Mkurugenzi wa Halmashauri atawasilisha taarifa ya mwenendo wa menejimenti na maamuzi yote yaliyofanyika kwenye kikao cha kwanza cha Baraza jipya la Madiwani baada ya uchaguzi,"

Na kuongeza kuwa “Matumizi mabaya ya madaraka au kushindwa kutekeleza majukumu kwa mujibu wa Notisi hizi kutamfanya Mkurugenzi kuwajibika binafsi kwa mujibu wa sheria,” amesisitiza.

Waziri wa TAMISEMI ametoa wito kwa wananchi wote, viongozi wa serikali, na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki kwa kuzingatia misingi ya Utawala Bora, Maadili ya Utumishi wa Umma na kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.


Aidha, ametoa pongezi na shukrani kwa Madiwani wote waliomaliza muda wao wa uongozi kwa mchango wao mkubwa katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yao na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment