WAKAGUZI WASAIDIZI WA MADINI WATAKIWA KUZINGATIA UBUNIFU NA UZALENDO KATIKA USIMAMIZI WA SEKTA YA MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 25, 2026

WAKAGUZI WASAIDIZI WA MADINI WATAKIWA KUZINGATIA UBUNIFU NA UZALENDO KATIKA USIMAMIZI WA SEKTA YA MADINI


Na Mwandishi Wetu - MOROGORO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amewataka Wakaguzi Wasaidizi wa Madini nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ubunifu, uzalendo na uadilifu ili kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amesema sekta hiyo ni miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo usimamizi madhubuti wa rasilimali za madini ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi.

Akizungumza wakati wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini na Wakaguzi Wasaidizi wa Madini kutoka maeneo mbalimbali nchini kilichofanyika mkoani Morogoro, Mhandisi Samamba amewataka watumishi hao kusimamia rasilimali za madini kwa uzalendo, akibainisha kuwa Serikali imewaamini kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa usimamizi wa sekta hiyo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujiepusha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuwa Sekta ya Madini ina vishawishi vingi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi na kwamba Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amewataka Wakaguzi Wasaidizi wa Madini kushirikiana kwa karibu na mamlaka nyingine za Serikali kuanzia ngazi ya vijiji, kata, wilaya na mikoa ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao na utatuzi wa changamoto zinazoweza kujitokeza katika maeneo ya shughuli za madini.

“Sambamba na ushirikiano huo, ninawataka kuhakikisha mnatoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za madini ili kuendelea kujenga taswira chanya ya Sekta ya Madini na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao,” amesema Mhandisi Samamba.

Pia amewataka viongozi na watendaji wa Tume ya Madini kuendelea kutoa mafunzo kwa Wakaguzi Wasaidizi wa Madini, hususan katika maeneo ya sheria, kanuni na taratibu za madini, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Wakati huo huo, Mhandisi Samamba amepongeza mchango wa Wakaguzi Wasaidizi wa Madini katika kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo, hatua iliyochangia ongezeko la makusanyo ya maduhuli pamoja na kupungua kwa ajali katika maeneo ya migodi.

“Kwa mfano, katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi sasa, Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi trilioni 1.36, sawa na asilimia 113.34 ya lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, huku ninyi mkiwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo kupitia kazi zenu za ukaguzi na usimamizi wa shughuli za madini,” amesema.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini pamoja na Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, wamewapongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya sekta hiyo na kuwataka kuendelea kuwa walinzi wa rasilimali za madini za Taifa.


Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, ameishukuru Wizara ya Madini kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kupitia upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kazi, ikiwemo magari na mashine za kisasa za kupima madini ya metali.

Amesema Tume ya Madini itaendelea kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia uboreshaji wa uwezo na usimamizi makini wa Wakaguzi Wasaidizi wa Madini nchini. 

No comments:

Post a Comment