TANZANIA NA URUSI KUIMARISHA SEKTA YA NISHATI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 21, 2025

TANZANIA NA URUSI KUIMARISHA SEKTA YA NISHATI


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev kuhusu kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati na maeneo mengine muhimu ikiwemo teknolojia na uwekezaji.

Mazungumzo hayo kati ya Dkt. Biteko na Mhe. Tsivilev yamefanyika kando ya Jukwaa la Kimataifa la Uchumi St. Petersburg nchini Urusi.

Kupitia mkutano huo Dkt. Biteko amesema kiwango cha uwekezaji nchini kutoka Urusi kinafikia dola za Kimarekani milioni 424 kupitia miradi 44 inayoajiri watu zaidi ya 3,000 huku akielezea fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya nishati.

"Tanzania ina asilimia 61.7 ya nishati kutoka vyanzo vinavyoweza kurejeshwa na fursa za uwekezaji zenye thamani ya dola bilioni 4 katika sekta ya nishati," amesema Dkt. Biteko.

Ametaja jitihada za Serikali katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya nishati sambamba na kushirikisha sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi ya pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akitolea mfano Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika Dar es Salaam mwezi Januari 2025 uliolenga kutoa umeme kwa waafrika milioni 600 ambao hawana umeme.

Pia, Dkt. Biteko amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Urusi kuongeza uwekezaji nchini hususan katika nishati safi ya kupikia ambapo ameelezea uwepo wa fursa za uwekezaji wa sekta binafsi za uzalishaji umeme wa kujitegemea na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amefurahishwa na uhusiano wa kidiplomasia wa takribani miaka 64 kati ya Tanzania na Urusi na kusema kuwa uhusiano huo unalenga kunufaisha wananchi wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev amezungumzia umuhimu wa nishati katika maendeleo ya kiuchumi hususan katika masuala ya usalama wa nishati, upatikanaji, bei nafuu, na ufanisi. 

Mhe. Tsivilev amesema kuwa Urusi ipo tayari kusaidia teknolojia na kujengea uwezo wataalamu wa Afrika ikiwemo Tanzania ili kuhakikisha uhuru wa teknolojia unakuwepo.

"Urusi ina mkakati wa haki katika ushirikiano na malengo ya kuendeleza mifumo ya nchi kwa washirika wa muda mrefu," amesema Mhe. Tsivilev.

Amezungumzia maeneo mengine ambayo Urusi imeahidi kuisaidia Tanzania ni pamoja na afya, usalama wa mtandao na ulinzi wa miundombinu muhimu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INTER RAO Export, ambayo ni moja ya Kampuni kubwa zaidi ya nishati duniani, Bw. Maxim Sergeev licha ya kuonesha nia ya kuwekeza nchini amesema kuwa Kampuni hiyo ina uwezo wa kutengeneza vifaa mbalimbali ikiwemo mashine umba na jenereta pia ina mikataba ya kila mwaka inayofikia dola bilioni 8.

Aidha, mazungumzo hayo kati ya Dkt. Biteko na Tsivilev yamehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania Moscow, Mhe. Frederick Kibuta, Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi John Ulanga na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Petroli, Mhandisi Marwa Petro.

Kando ya mazungumzo hayo naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange amefanya mazungumzo na Kampuni ya Rosatom na Unigreen kuhusu ushirikiano wa uzalishaji wa umeme unaotokana na urani pamoja na jua ambapo Unigreen inaendelea na taratibu za uwekezaji nchini.

No comments:

Post a Comment