TUZO ZA DUNIA ZA UTALII KUFANYIKA TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 26, 2025

TUZO ZA DUNIA ZA UTALII KUFANYIKA TANZANIA



Na Mwandishi Wetu,
Dodoma


Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana (Mb.), amesema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za Dunia za Utalii (World Travel Awards) Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi kwa mwaka 2025, hafla inayotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi, tarehe 28 Juni 2025, jijini Dar es Salaam.

Balozi Dkt. Chana ametoa taarifa hiyo Juni 26,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo ameeleza kuwa tukio hilo linathibitisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya utalii duniani, na ni matokeo ya juhudi kubwa za serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia kampeni ya Tanzania: The Royal Tour na juhudi nyingine zinazolenga kukuza na kutangaza utalii.

“Tanzania kuwa mwenyeji wa tukio hili la kimataifa ni uthibitisho wa hadhi kubwa ambayo nchi yetu imejipatia kimataifa katika sekta ya utalii,” alisema Balozi Chana kwa msisitizo.

Tuzo hizo, zilizoanzishwa mwaka 1993 nchini Uingereza chini ya kampuni ya World Luxury Media Group, zinalenga kutambua na kutoa heshima kwa watoa huduma bora za utalii. Kwa miaka 32 mfululizo, zimekuwa jukwaa rasmi la kuonesha ubora wa huduma, vivutio, na mafanikio ya nchi mbalimbali duniani katika sekta ya utalii.

Balozi Dkt.Chana amesema Tanzania ilianza kushiriki tuzo hizo mwaka 2013, na kwa kipindi cha miaka michache iliyopita, imeibuka kidedea mara kadhaa, ikiwemo tuzo ya Kivutio Bora Barani Afrika kwa Mlima Kilimanjaro na tuzo tano mnamo mwaka 2024 pekee, hatua ambazo zinaonyesha wazi mafanikio ya dhahiri ya sekta hiyo nchini.

Amesema kwa mwaka huu wa 2025, Tanzania imeingia katika mashindano ya vipengele zaidi ya 50, ikiwemo: Eneo Bora la Utalii Afrika, Bodi Bora ya Utalii, Hifadhi Bora Afrika, Kampuni Bora za Safari, na Hoteli Bora kwa Watalii. Ushiriki huo umetokana na ushirikiano wa karibu kati ya sekta za umma na binafsi, ukilenga kuendeleza ubora wa huduma na vivutio vya utalii nchini.

Aidha, tukio hilo linatarajiwa kuvuta zaidi ya wageni 250 kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo wawekezaji, waandishi wa habari wa kimataifa, wawakilishi wa kampuni za ndege, hoteli, mashirika ya usafirishaji, na wadau wengine wakubwa wa utalii barani Afrika na visiwa vya Bahari ya Hindi.

“Tanzania Shines 2025 – kwa pamoja tuitangaze Tanzania, kwa pamoja tuendelee kuifanya Tanzania kuwa isiyosahaulika,” alisisitiza Balozi Chana





No comments:

Post a Comment