MAVUNDE AAGA UBUNGE KWA KISHINDO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 26, 2025

MAVUNDE AAGA UBUNGE KWA KISHINDO


Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Mhe Anthony Mavunde, leo Juni 26, 2025, ametangaza rasmi kuhitimisha safari yake ya miaka kumi ya kulitumikia Jimbo la Dodoma Mjini, huku akiacha alama kwa kuzindua mfumo wa kidigitali wa kupokea na kushughulikia kero za wananchi pamoja na kugawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222.

Akizungumza kwa hisia mbele ya viongozi wa mitaa, wananchi na wataalamu wa TEHAMA waliokusanyika jijini Dodoma, Mavunde amesema ameamua kuondoka kwenye nafasi ya ubunge akiwa hana deni kwa wananchi waliompa dhamana ya uongozi kwa muongo mmoja.

 “Leo ndiyo siku yangu ya mwisho kama Mbunge wa Dodoma Mjini,nawashukuru kwa kuniamini na kunipa heshima ya kuwa kiongozi wenu kwa miaka kumi. Nimejitahidi kuishi kama mtumishi wa watu, si kiongozi wa majukwaa tu,” amesema kwa sauti ya utulivu.

Katika hatua ya kuimarisha uwajibikaji wa viongozi wa msingi na kuendeleza misingi ya utumishi aliyojijengea, Mavunde amezindua mfumo maalum wa TEHAMA unaowezesha wenyeviti wa mitaa kupokea kero za wananchi kwa wakati na kuzifikisha kwa wahusika husika, bila kuchelewa.

Amesema mfumo huo, ambao ni wa kwanza kuanzishwa katika ngazi ya jimbo nchini, utaunganishwa katika kata zote 41 za Dodoma Mjini na utaendelea kutumika hata baada ya yeye kuondoka madarakani.

 “Mfumo huu utawasaidia viongozi wote kupokea taarifa kwa wakati mmoja,hata mbunge akipigiwa simu na kukosekana, ujumbe hautapotea,tumeingia kwenye zama za utawala wa kidigitali,” ameeleza.

Kwa mujibu wa Mavunde, kila mwenyekiti wa mtaa atapewa simu janja ya kutumia kama chombo cha kazi, akisisitiza kuwa si kifaa cha anasa bali ni zana ya kuwahudumia wananchi.

 Ameeleza kuwa simu hizo zimetengenezwa katika kiwanda cha ndani kilichopo Mkuranga, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya viwanda.

Aidha, Mavunde ametoa wito kwa Mbunge atakayechukua kijiti baada yake kuendeleza mfumo huo na kukamilisha ahadi zilizotolewa kwa wananchi wa Dodoma Mjini.

“Nitahakikisha nashirikiana vyema na mbunge atakayekuja, ataelekezwa vizuri kuhusu mfumo huu ili asije kuutatua kero za wananchi,nataka historia ya utumishi wa kweli iendelee,sitaki kuondoka nikiwa na deni kwa watu wangu,” amesema kwa msisitizo.

Akieleza sababu ya kuwa mstari wa mbele kutatua changamoto za msingi, Mavunde amegusia namna alivyosukumwa na maumivu ya kuona wananchi wake wakihangaika na usafirishaji wa miili ya wapendwa wao  hali iliyomfanya kununua gari maalum kusaidia shughuli hiyo.

 “Nilishuhudia mtu akibeba maiti kwenye pikipiki. Hilo lilinigusa sana. Nilichukua uamuzi wa kununua gari la kusaidia misiba badala ya kutoa michango kila siku. Nilitukanwa sana lakini sasa wananchi wananufaika,” alisimulia kwa hisia.

Katika kuhitimisha hafla hiyo, Mavunde ametangaza kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha SACCOs ya wenyeviti wa mitaa wa Dodoma Mjini, ili kuwawezesha kiuchumi na kuwaongezea motisha ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

“Siku zote tutabaki kuwa pamoja. Tutatenganishwa na mipaka ya kijiografia tu, lakini dhamira ya kuhudumia watu haitapotea,” amesema

No comments:

Post a Comment