WAZIRI GWAJIMA AZINDUA MADAWATI YA HUDUMA ZA USTAWI JAMII KATIKA VITUO VYA USAFIRISHAJI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 30, 2025

WAZIRI GWAJIMA AZINDUA MADAWATI YA HUDUMA ZA USTAWI JAMII KATIKA VITUO VYA USAFIRISHAJI.



Na WMJJWM - Dar Es Salaam


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua rasmi Mwongozo wa Taratibu za Utoaji wa Huduma za Ustawi wa Jamii kwa Watoto Wanaoishi na Kufanya Kazi Mitaani pamoja na Dawati la Huduma katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli Juni 30, 2025 Jijini Dar Es Salaam.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kwa vitendo kukomesha tatizo la watoto wanaokimbilia mitaani kutokana na changamoto za kifamilia, kiuchumi na kijamii.

Amesema takwimu zilizotolewa zinaonesha kuwa zaidi ya watoto 10,000 waliokolewa kati ya Julai 2024 hadi Juni 2025 kupitia kampeni maalum ya kitaifa. Mwongozo huo utasaidia watoa huduma kwenye vituo vya usafiri kubaini viashiria vya hatari kama vile ukatili usafirishaji haramu na utoroshwaji wa watoto mapema, hivyo kuwaokoa kabla hawajazama katika maisha ya mitaani.

"Mtoto hana mtaa hivyo anapaswa kuwa mikononi mwa familia na jamii yake. Tuungane kwa dhati kumaliza tatizo hili kwa vitendo na si kwa maneno tu" amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima

Serikali pia imeanzisha Madawati 14 ya Ustawi wa Jamii katika vituo vya usafirishaji kwenye mikoa 11 nchini ikiwepo Tabora, Mbeya, Dodoma, Kagera, Arusha, Morogoro, Songea, Shinyanga (2), Njombe, Mwanza(2) na Dar Es Salaam ili kutoa msaada kwa watoto na makundi maalum wanaokumbana na changamoto mbalimbali wakiwa safarini au wanapofika mijini.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema umuhimu jamii kuwekeza katika Ustawi na Malezi ya watoto na kutoa rai kwa kila mwanajamii kutimiza wajibu katika sehemu yake.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI Subisya Kabuje amesema wataendelea kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kuhakikisha huduma za ustawi wa jamii zinafikiwa na kila mwananchi kwa kufuatilia utendaji kazi wa madawati haya ipasavyo.

Aidha Mwakilishi wa Balozi wa Umoja wa Uingereza Bw.Felix Wood ameeleza kwamba uongezekaji wa miundombinu ni jambo zuri katika nchi lakini pia huchochea ongezeko la watoto wanaokimbilia kuishi na kufanya kazi katika mazingira hatarishi hivyo kutoa rai kwa wadau wote wa maendeleo kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wanakuwa sawa na kupata malezi bora kutoa katika familia zao kabla ya kukimbilia mtaani.













No comments:

Post a Comment