Na WMJJWM-Dodoma.
Serikali inaendelea na juhudi kuhakikisha inawalinda Watoto dhidi ya maudhui yanayoweza kuwapotezea dira na muelekeo wa maisha mtandaoni ili kuweza kujenga taifa lenye maadili na watu wanaojitambua.
Hayo yamebainishwa na Naibu katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju katika kikao kazi cha kamati ya Taifa ya ushauri juu ya usalama na ulinzi wa watoto mitandaoni kilichofanyika Julai 09,2025 Jijini Dodoma.
Wakili Mpanju amefafanua kwamba elimu ya kuwalinda watoto mtandaoni ni muhimu kutolewa kwa jamii hususan kwa wazazi, walezi na walimu ilikupata uelewa na wao waweze kuwekeza juhudi katika vita ya kumlinda mtoto dhidi ya madhara anayoweza kupata mtoto anapotumia vifaa vya kielektroniki ipasavyo.
“Ni lazima tuielimishe jamii juu ya mabadiliko ya teknolojia kupitia majukwaa sahihi ili kuwalinda watoto kwani wao ndiyo wanaokaa nao muda mwingi lakini vilevile utekelezaji wa sheria bila kuwa na elimu juu ya masuala haya tutakuwa hatujatimiza wajibu wetu “amesema Mpanju.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka wizara ya Maendeleo ya Jami,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku amesema kikao kazi hicho kimedhamiria kukamilisha mpango kazi wa Taifa juu ya matumizi ya laini za simu za watoto ili mamlaka husika ziweze kufuatilia mienendo ya watoto na kuwa rahisi kutambua pale ambapo watoto wanapokua hatarini.
Naye mkurugenzi msaidizi wa huduma za ustawi wa jamii kutoka Ofisi ya Rais- Tamisemi Subisya Kabuje amesema ofisi ya Rais-Tamisemi itashirikiana na Wizara ya Maendeleo yq Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum kuhakikisha watoto wanakuwa salama kupitia Kuratibu utekelezaji wa afua za kumlinda mtoto mtandaoni katika tawala za Mikoa na Serikali za mitaa kwa kuhakikisha mifumo inasomana na kurahisisha zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment