Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa madhehebu ya dini nchini kuendelea kuliombea Taifa ili kudumisha amani na utulivu uliopo pamoja na kutekeleza mipango yao ya maendeleo inayolenga kuihudumia jamii kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito huo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipomwakilisha katika Uzinduzi wa Harambee ya Ujenzi wa Ofisi Kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, iliyofanyika katika eneo la mradi-Nzuguni C, Jijini Dodoma.
Akitoa salamu hizo za Mhe. Rais, Dkt. Nchemba alisisitiza umuhimu wa wananchi wote kuwaepuka watu ama makundi ya watu waliodhamiria kuvuruga amani ya nchi kwa sababu bila amani nchi haiwezi kupata maendeleo kama ambavyo hivi sasa nchi inavyopiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wote wakiwemo waumini wa dini na madhehebu mbalimbali kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili kutimiza wajibu wao wa kidemokrasia wa kuchagua na kuchaguliwa.
Aidha, Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa, Serikali inatambua mchango mkubwa wa madhehebu ya dini katika maendeleo ya nchi kutokana na huduma mbalimbali za kiroho na kimwili zinazotolewa na Taasisi hizo ikiwemo afya, elimu na maji.
Alisema kuwa katika kuunga mkono ushirikiano huo, Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanyiakazi changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na Viongozi wa Dini ikiwemo kusamehe kodi kwenye vitu vinavyoagizwa na madhehebu ya dini na kwamba ushirikiano huo utanedelea kudumishwa.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mipango, Uchumi na Utaweala wa Kanisa la Kiinjuili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Dodoma, CPA Edmund Mugasha alisema kuwa zaidi ya shilingi bilioni 10 zinahitajika kutekeleza mradi huo na kwamba tayari waumini wa Kanisa hilo wamechanga zaidi ya shilingi milioni mia sita kupitia michango na sadaka zao.
Alisema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo mkubwa inatarajia kutumia shilingi bilioni 3 na kwamba mradi huo umepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka 7.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kiingili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, Baba Askofu Dkt. Christian Ndossa, aliishukuru Serikali kwa mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Taasisi za dini nchini.
Aidha, aliiomba Serikali itatue baadhi ya changangamoto za mradi huo ikiwemo maombi ya kurejeshewa eneo la mita za mraba elfu 28 ambazo zilimegwa na wananchi waliovamia eneo lao na kuahidiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwamba wangerejeshewa eneo hilo.
Katika Harambee hiyo inayokusudia kupata fedha za kujenga Ofisi za Makao Makuu ya Dayosisi ya Dodoma na Jengo la Kitega uchumi, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amechangia shilingi milioni 50 huku Dkt. Nchemba akichangia shilingi milioni 25 na kuendesha Harambee ambapo kiasi kilichopatikana ni shilingi milioni 173.5 kikihusisha ahadi ya shilingi 159.7 na fedha taslimu shilingi milioni 13.8 pamoja na vifaa vya ujenzi.
No comments:
Post a Comment