
Na Okuly Julius, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa zaidi ya shilingi bilioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta za elimu, miundombinu ya barabara, nishati, na reli.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Macha amesema kati ya mwaka 2020 hadi 2025 Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 119.9 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu mkoani humo.
“Katika kipindi hiki, fedha hizo zimetumika kujenga na kukamilisha miundombinu mbalimbali ya shule za msingi, sekondari na vyuo, hatua iliyosaidia kuongeza upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wa ngazi zote,” amesema.
Ameongeza kuwa bajeti ya elimu bila ada kwa shule za msingi na sekondari imeongezeka kutoka shilingi bilioni 6.81 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 37.7 mwaka huu. Aidha, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 513 mwaka 2020 hadi 611 mwaka 2025, huku shule za sekondari zikiongezeka kutoka 167 hadi 197 katika kipindi hicho.
Macha ametaja baadhi ya shule zilizojengwa kuwa ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Bweni ya Wasichana ya Mkoa wa Simiyu, iliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 na kuzinduliwa rasmi na Rais Dkt. Samia.
Kuhusu sekta ya barabara, Macha alisema Mkoa wa Simiyu umepokea shilingi bilioni 257.5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo, ambapo shilingi bilioni 70.4 zimetekeleza miradi ya TARURA na shilingi bilioni 187.1 miradi ya TANROADS.
Aidha, amezungumzia ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,596, ambapo kipande cha tano chenye urefu wa kilomita 341 kinapita mkoani Simiyu.
“Ujenzi wa kipande hiki ulianza Mei 15, 2021 kwa gharama ya shilingi trilioni tatu. Kukamilika kwa reli hii kutapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo, bidhaa na abiria, sambamba na kupunguza uharibifu wa barabara,” ameeleza Macha.

Akizungumzia sekta ya nishati, Macha amesema jumla ya shilingi bilioni 130.8 zilitolewa kati ya mwaka 2020 hadi 2025 kwa ajili ya usambazaji wa huduma ya umeme mkoani humo.
Pia, alisema ujenzi wa kituo kikubwa cha kupoza umeme unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 49, huku Serikali ikilenga kuunganisha umeme katika kaya 231,850 kati ya 317,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia mpango wa National Energy Compact.
Katika hatua nyingine, Macha alisema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kusambaza majiko ya gesi kwa ruzuku ya asilimia 50.
“Majiko 16,605 ya gesi kilo sita yamesambazwa kwa ruzuku ya shilingi milioni 332.1. Taasisi nne za elimu zikiwemo shule za sekondari za wasichana Simiyu, Maswa, Nyalanja na Mkula zimefungiwa majiko ya gesi ya kisasa na kuachana na kuni kabisa,” amesema.
Macha alihitimisha kwa kusema kuwa mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wa mikoa yote kwa usawa, ikiwemo mikoa ya pembezoni kama Simiyu.
No comments:
Post a Comment