Na Bahati Mollel – Dodoma
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Maabara yake ya Mkoa wa Dodoma, imewahamasisha wakandarasi, taasisi za serikali na wajenzi binafsi kutumia huduma za upimaji wa malighafi kwa gharama nafuu kabla ya kuanza au kuendelea na miradi ya ujenzi wa miundombinu.
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Vifaa na Vipimo wa Maabara hiyo, Mhandisi Faustine Makumbi, ambaye amesema maabara hiyo inatoa huduma za kitaalamu katika upimaji wa ubora wa malighafi zinazotumika kwenye ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu mingine muhimu.
“Tunaweza kusaidia wajenzi kubaini kama malighafi zao zinakidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuanza matumizi. Hii husaidia kuepuka hasara na kuchangia ujenzi wa miundombinu imara na ya kudumu,” amesema Mhandisi Makumbi.
Ameeleza kuwa maabara hiyo inatumia vifaa vya kisasa, ikiwa ni pamoja na mashine ya nyuklia (Troxler) inayopima kiwango cha mgandamizo moja kwa moja kwenye eneo la kazi, na mbinu ya “sand replacement” inayohusisha uchambuzi wa kina wa sampuli za udongo au mchanga.
Kwa upande wake, Fundi Sanifu Msaidizi wa Maabara, Bw. Adolf Ngawambara, amesema maabara hiyo pia ina uwezo wa kupima lami kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ambapo lami hutenganishwa na kokoto kwa kutumia petroli, na kokoto hukauka kwa muda wa saa tatu hadi nne ili kutoa taarifa sahihi kuhusu ubora wa lami.
Mhandisi Msaidizi wa Maabara, Bw. Joel Sanga, ameongeza kuwa vipimo vya kokoto dhidi ya mshtuko na mkandamizo vinafanyika kwa kutumia mashine maalum baada ya kokoto kukatwa kwa vipimo sahihi vya milimita 10, hatua ambayo ni muhimu kuhakikisha uimara wa ujenzi.
Naye Bi. Stella Chedego, Fundi Sanifu anayehusika na vipimo vya udongo, amesema maabara hupima tabia za udongo kwa kuuhifadhi kwa saa 24 ili kubaini viambato kama maji na plastiki, ambavyo huathiri utendaji wa udongo kwenye ujenzi.
Kwa upande mwingine, Bw. Kaja Kisiwa, Fundi Sanifu Msaidizi, ameeleza kuwa maabara hiyo hufanya majaribio ya mshindilio wa barabara baada ya hatua za awali za usawazishaji ili kuhakikisha uthabiti na uimara wa barabara inayojengwa.
Akihitimisha, Mhandisi wa Maabara, Bi. Getrude Enock, ametoa wito kwa wajenzi wote, wa sekta ya umma na binafsi, kutumia kikamilifu huduma za maabara hiyo.
“Tunakaribisha wajenzi wote kuja kupima malighafi zao hapa. Tuna vifaa vya kisasa, matokeo ya haraka, na gharama zetu ni nafuu. Kupima ni hatua muhimu ya kuhakikisha miundombinu tunayojenga ni salama, bora na ya kudumu—kwa maendeleo ya taifa,” amesema Bi. Getrude.
Kwa maelezo zaidi kuhusu huduma za maabara ya TANROADS mkoa wa Dodoma, wananchi wanahimizwa kuwasiliana na ofisi ya TANROADS Dodoma au kutembelea maabara hiyo iliyopo katika eneo la ofisi za TANROADS mkoani humo.
No comments:
Post a Comment