
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Canada katika kuboresha sekta ya elimu, hususan elimu ya ualimu na ufundi stadi.
Akizungumza jijini Dodoma tarehe 21 Julai 2025, baada ya kikao na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Mhe. Randeep Sarai, Prof. Mkenda amesema Canada imeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya elimu kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali.
Amesema katika kikao hicho, wamejadili kwa kina ushirikiano uliopo na miradi inayoendelea kutekelezwa, huku wakitilia mkazo umuhimu wa kutoa fursa kwa Watanzania kupata mafunzo katika vyuo mahiri vya Canada.

Miongoni mwa miradi iliyofadhiliwa na Serikali ya Canada ni:Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) wenye thamani ya TZS bilioni 92,Mradi wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP) wenye thamani ya TZS bilioni 47,Mradi mpya wa Maendeleo Endelevu katika Elimu ya Ualimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TESDP) utakaoigharimu Canada takriban TZS bilioni 37.

Kwa upande wake, Mhe. Randeep Sarai alieleza dhamira ya Canada ya kuendelea kuwekeza katika maeneo ya kijamii, likiwemo Mpango wa Lishe Shuleni unaolenga kuboresha afya za wanafunzi kwa lengo la kuongeza uandikishaji, mahudhurio na ufaulu. Mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani milioni 12.
Aidha, alibainisha kuhusu Mradi wa BLOOM unaolenga kuwawezesha wanawake na wasichana kupitia mafunzo ya ujuzi chini ya VETA, wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 20.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Nombo, alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na NMB Foundation inatekeleza mradi wa kuwawezesha wahitimu wa VETA kuingia katika soko la ajira kupitia programu maalum ya mafunzo ya ujasiriamali, nafasi za mafunzo kwa vitendo viwandani na utoaji wa vifaa vya kuanzishia biashara (startup kits).
Amesema hatua hiyo itaunganishwa na mradi mpya unaotekelezwa na taasisi ya FINCA kwa ufadhili wa Serikali ya Canada, ili kuhakikisha vijana wanatumia stadi walizopata kujiajiri na kuchangia uchumi wa nchi.
Prof. Nombo alisisitiza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha elimu ya ufundi stadi inakuwa chachu ya maendeleo na ajira kwa vijana nchini.



















No comments:
Post a Comment