
Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Jengo jipya la Makao Makuu ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) linalojengwa katika eneo la Kilimani Jijini Dodoma linatarajiwa kuongeza fursa kwa wabunifu na kampuni atamizi, hususan kutoka Jijini Dar es Salaam, kwa kuwa na kumbi za kutosha kwa ajili ya kuendeleza ubunifu katika sayansi na teknolojia.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, jengo hilo litagharimu takribani Shilingi bilioni nane hadi kukamilika kwake, fedha ambazo zinatolewa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza mazingira ya ubunifu na kutoa nafasi za kutosha kwa vijana na watafiti kuendeleza kazi zao.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa COSTECH, Profesa John Kondoro, amesema kuwa Bodi, Menejimenti na Maofisa wa COSTECH wameridhishwa na kasi, thamani na ubora wa ujenzi wa jengo hilo, unaoendelea kwa haraka.
Amesema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 15, ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu mbele ya ratiba, hali inayodhihirisha utendaji mzuri wa mkandarasi.
Mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya TIL LTD, alikabidhiwa eneo la ujenzi mwezi Machi mwaka huu, na kwa mujibu wa Mhandisi Razack William kutoka kampuni hiyo, jengo hilo litakabidhiwa rasmi kwa COSTECH Machi 24, 2026, kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa miezi 12.
Kwa upande wake, Msanifu Majengo kutoka Kampuni ya Mekon Consult Ltd, Benedict Martin, alieleza kuwa jengo hilo mbali na kuwa ofisi za makao makuu ya COSTECH, litakuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo kumbi za wabunifu na atamizi zitakazosaidia kukuza ubunifu, hasa kwa vijana.
Ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha miundombinu ya taasisi muhimu kama COSTECH, ili kuharakisha maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia nchini.









No comments:
Post a Comment