
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro, akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 19, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo jijini Dodoma, kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Mkoa huo.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG Dodoma
MKOA wa Kigoma umeendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya utalii, kilimo, madini na mazingira, hatua iliyochochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira mkoani humo.
Akizungumza Julai 19, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro, alisema juhudi za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimezaa matunda makubwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Katika sekta ya utalii, Sirro amesema watalii wa ndani wameongezeka kutoka 630 mwaka 2020 hadi 11,769 mwaka 2025, huku watalii wa nje wakiongezeka kutoka 345 hadi 655. Mafanikio haya yamechangiwa na kutangazwa kwa vivutio vya kipekee kama Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Mahale, Ziwa Tanganyika, na Kituo cha Kumbukumbu cha Dk. Livingstone kilichopo Ujiji.
Katika sekta ya kilimo, Mkoa wa Kigoma umeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa zao la chikichi, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 25,000 mwaka 2020/2021 hadi tani 35,000 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 40.
Amesema uzalishaji wa mbegu bora za chikichi aina ya TENERA umeongezeka kutoka milioni 1.6 hadi milioni 2.9 – ongezeko la asilimia 85.4. Serikali pia imenunua pikipiki 153, vipima udongo 5 na magari 2 kwa ajili ya maafisa ugani, ambapo watumishi wapya 93 wameajiriwa na wengine 7 kupangwa kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT).
Matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 21,780 hadi tani 40,296 sawa na ongezeko la asilimia 85. Aidha, vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka kimoja hadi vinane, sawa na ongezeko la asilimia 700, jambo lililoboresha upatikanaji wa masoko, mikopo na usimamizi wa rasilimali kwa wakulima.
Serikali imejenga nyumba 4 za watumishi wa sekta ya kilimo katika vijiji mbalimbali kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kazi na kuongeza uwepo wa wataalamu wa kilimo mashinani.
Kwa upande wa sekta ya madini IGP Mstaafu Sierra amesema, uzalishaji wa dhahabu umeongezeka kutoka gramu 12,500 mwaka 2020 hadi gramu 15,200 mwaka 2025 – ongezeko la asilimia 22. Mauzo ya madini nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani 22,600 hadi 115,400 – ongezeko la asilimia 411.
Masoko ya madini yameongezeka kutoka soko moja (Kakonko) hadi masoko mawili (Kakonko na Kigoma), huku leseni za uchimbaji zikiongezeka kutoka 354 hadi 799.
Katika kulinda na kuendeleza mazingira, Mkoa wa Kigoma umefanikiwa kuhifadhi misitu ya vijiji 141 yenye ukubwa wa hekta 91,691 na usimamizi wa misitu ya halmashauri tatu zenye hekta 208,556. Aidha, misitu 13 ya Serikali Kuu yenye ukubwa wa hekta 222,919 na kitalu cha uwindaji cha Makere-Uvinza chenye hekta 100,000 vimeendelezwa.
Katika juhudi za kuendeleza hifadhi za nyuki, misitu 7 ya vijiji imetengwa kwa ajili ya shughuli hizo, huku Halmashauri ya Uvinza ikiingia mkataba wa kuuza hewa ya ukaa kutoka Msitu wa Masito.
Serikali pia imetoa hekta 10,000 za ardhi kutoka Msitu wa Makere Kusini kwa ajili ya kilimo na ufugaji kwa wananchi wa Mvinza, Kagerankanda na maeneo ya Halmashauri.
Kwa kushirikiana na wadau wa mazingira, Mkoa wa Kigoma umepanda jumla ya miti milioni 34.5 kati ya mwaka 2020 hadi 2025 katika wilaya zote, ili kuhifadhi vyanzo vya maji, kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


No comments:
Post a Comment