BASHUNGWA AHIMIZA VYAMA VYA SIASA KUSHIRIKI KAMPENI ZA UCHAGUZI BILA KUHATARISHA AMANI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 22, 2025

BASHUNGWA AHIMIZA VYAMA VYA SIASA KUSHIRIKI KAMPENI ZA UCHAGUZI BILA KUHATARISHA AMANI.



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amevihimiza Vyama vya Siasa pamoja na Wagombea wa Urais, Ubunge na Udiwani kunadi sera zao kwa Wananchi bila kutumia lugha ya matusi au kuanzisha vurugu zinazoweza kuhatarisha amani, pia amewasisitiza Wananchi kushiriki katika shughuli za kisiasa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu na kushiriki kupiga kura Oktoba 29, 2025.

Bashungwa ametoa wito huo leo, tarehe 22 Agosti 2025, mara baada ya kuzindua jengo la Kituo cha Polisi Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa jukumu la ulinzi wa Taifa ni la Watanzania wote, siyo Serikali, Jeshi la Polisi au vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

“Wananchi wote muwe huru kushiriki katika shughuli za siasa hususan wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, zitakazoanza wiki ijayo pamoja nasiku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025. Ni matumaini yangu kwamba vyama vya siasa na wagombea wao wa Uraisi, Ubunge, Udiwani watajielekeza kunadi sera zao, na sio matusi ama kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani.” amesema Bashungwa.

Waziri Bashungwa amewahakikishia Wananchi kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, hivyo akawahimiza kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii bila kuwa na hofu yoyote.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya taasisi, watu binafsi pamoja na vikundi vya watu ambao wamekuwa wakitoa taarifa zinazolenga kuleta taharuki na hofu ya kiusalama nchini, hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Ameliagiza Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na Vyombo vya Usalama, kuendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa wale watakaokaidi na kutaka kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Halima Okash, amesema kukamilika kwa Kituo cha Polisi cha Wilaya kutasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao, pamoja na kuwezesha Maafisa na Askari wa Jeshi hilo kutimiza majukumu yao katika mazingira mazuri.

Awali, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi (DCP), Narsis Misama amesema ujenzi wa Kituo cha Polisi Chemba cha Daraja B ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeliwezesha Jeshi la Polisi kuitekeleza ili kuendelea kuboresha mazingira ya Jeshi hilo kutekeleza majukumu yake.









No comments:

Post a Comment