Watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Singida wameahidi kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira pamoja na kuokoa afya za wananchi.
Wametoa ahadi hiyo leo wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 395 kwa watumishi wa jeshi hilo Mkoa wa Singida iliyoongozwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Sophia Mgonja aliyekuwa ameambatana na Mjumbe mwingine wa Bodi hiyo, Wakili Mwantumu Sultan.
“Tunapenda kumshukuru Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa fedha zilizowezesha kufungiwa nishati safi ya kupikia katika magereza zetu na kwa sasa hatutumii tena kuni.
Na sasa akaona atukumbuke na watumishi. Kwa kweli tunashukuru sana na tunaahidi kuwa mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia kwa jamii inayotuzunguka,” amesema ACP. Felix Mwakyusa, Mwakilishi wa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida.
Awali akizungumza na Maafisa pamoja na Askari wa jeshi hilo, Mhandisi Mgonja amesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia licha ya kuokoa afya za wanaotumia, lakini pia inasaidia kuokoa na kulinda mazingira.
“Tumekuwa tukipata changamoto za kimazingira kama upungufu wa mvua na ukame baadhi ya sehemu. Na hii inatokana na kukata miti kwa ajili ya matumizi ya kupikia. Kwa kutumia nishati safi ya kupikia tunakwenda kulinda na kuokoa mazingira yetu. Niwaombe tukawe mabalozi kwa ndugu, jamaa pamoja na jamii zinazotuzunguka ili wote tuhamie kwenye nishati safi ya kupikia,” amesema Mhandisi Mgonja.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa ugawaji wa majiko hayo ni muendelezo wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na REA kuhakikisha maono ya Mhe. Rais pamoja na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umebainisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia unafikiwa.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mtaalam wa Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali amesema kuwa jumla ya mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 395 yanatarajiwa kugaiwa kwa watumishi wa jeshi hilo Mkoa wa Singida.
No comments:
Post a Comment