Maagizo ya Rais Samia ya kujengwa kwa Makumbusho Kongwa yaanza kutekelezwa - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 14, 2025

Maagizo ya Rais Samia ya kujengwa kwa Makumbusho Kongwa yaanza kutekelezwa



Na Anangisye Mwateba, Kongwa


Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zimeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, la kujenga Makumbusho ya Taifa wilayani Kongwa, mkoani Dodoma.

Agizo hilo lilitolewa na Mhe. Rais Agosti 10, 2025, wakati wa ibada ya mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge, Job Ndugai, iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma. Rais Samia alielekeza kuwa makumbusho hayo yatakuwa kumbukumbu muhimu ya harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika na kielelezo cha mchango wa Tanzania katika historia hiyo.

Aidha, Mhe. Rais alisema kuwa eneo hilo liendelezwe kama sehemu ya utalii wa kihistoria, ikizingatiwa kuwa Hayati Ndugai enzi za uhai wake alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa makumbusho hayo ili kuhifadhi historia ya harakati za ukombozi.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, amesema eneo la Kongwa lina umuhimu wa pekee kihistoria, kutokana na kuwa sehemu ambayo marais watano wa nchi za kusini mwa Afrika waliwahi kuishi na kujifunza mbinu za kujikomboa kutoka katika utawala wa kikoloni.

“Wataalamu wetu wanapaswa kuandaa mkakati madhubuti wa kulifanya eneo hili kuwa kituo cha utalii endelevu na hifadhi ya kihistoria, kwa manufaa ya taifa letu na nchi nyingine ambazo zilitumia Kongwa kama kitovu cha harakati za ukombozi,” amesema Mhe. Kitandula.

Kwa upande wake, Ofisa Utamaduni Mwandamizi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Peter Maqway, ambaye ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, amesema kuwa kituo cha uhifadhi wa historia ya harakati za ukombozi kilianzishwa kwa lengo la kutambua, kulinda na kuendeleza historia hiyo adhimu ya Bara la Afrika.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Mayeka Saimon Mayeka, alizishukuru wizara zote mbili kwa kuitikia agizo la Rais kwa haraka, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kufungua fursa za utalii na utafiti wilayani humo.

“Makumbusho haya yatakuwa kivutio cha kitaifa na kimataifa na yataimarisha utalii wa kihistoria pamoja na uchumi wa eneo letu,” amesisitiza Mkuu huyo.










No comments:

Post a Comment