Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Wilson Mulumbe, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuiongoza nchi ataondoa madeni ya mikopo ya elimu ya juu yanayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, pamoja na kuhakikisha wananchi wote wanaunganishiwa umeme bure.
Mulumbe amesema pia ataweka Mfuko wa Msaada wa Mtoto utakaosaidia malezi kuanzia mtoto anapozaliwa hadi atakapofikisha miaka 18, pamoja na kuondoa gharama za kuunganishiwa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, akiwa ameambatana na mgombea mwenza Shoka Khamis Juma, Mulumbe amesema ndani ya miezi mitatu baada ya kuapishwa ataondoa madeni yote ya wahitimu wa vyuo vikuu.
Amesema ADC imeamua kuchukua hatua hiyo kwa kuwa wahitimu hao ni wataalamu ambao taifa linawategemea katika sekta mbalimbali za maendeleo.
"Nikiapishwa, ndani ya miezi mitatu nitafuta madeni yote ya wahitimu wa vyuo vikuu ambayo yanatokana na mikopo waliyopewa wakiwa vyuoni," amesema Mulumbe.
Aidha, amesema katika kipindi hicho pia wananchi wote wataunganishiwa umeme bure ili kuongeza matumizi ya umeme kutoka asilimia 37 ya sasa hadi asilimia 100.
Kuhusu Mfuko wa Msaada wa Mtoto, Mulumbe amesema utahakikisha mtoto analelewa na kusaidiwa na serikali hadi kufikisha miaka 18, kisha jukumu la malezi litaendelea kwa wazazi.
No comments:
Post a Comment