Timu za michezo ya SHIMIWI zaipania Utumishi SC katika soka - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 31, 2025

Timu za michezo ya SHIMIWI zaipania Utumishi SC katika soka



Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Klabu shiriki kwenye michezo ya 39 Shirikisho ya Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa nchini (SHIMIWI), kwa mchezo wa soka zimepania kuivua ubingwa timu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Utumishi SC katika michezo itakayoanza tarehe 1 hadi 16 Septemba, 2025 jijini Mwanza.

Viongozi mbalimbali wa klabu shiriki wamesema wamejiandaa vyema kwa ajili yakutwaa ubingwa wa michezo mbalimbali ukiwemo wa mpira wa miguu unaoshikiliwa na Utumishi SC, walioutwaa mwaka jana 2024 jijini Morogoro kwa kuwafunga Wizara ya Maji katika mchezo mkali wa fainali kwa penati 3-2 baada ya kumaliza muda wa kawaida wakiwa suluhu.

Bi. Debora Zera, Katibu wa RAS Geita amejinasifu kuwa timu yake ya mpira wa miguu inaviwango vya juu, kutokana na kufanya mazoezi kwa muda mrefu na anauhakika wa kufika fainali ya michezo hiyo.

“Kwa upande wa michezo tutashiri mikuu mitatu na mingine ya ndani, ila tunauhakika zaidi wa kutwaa ubingwa wa mpira wa miguu maana wapo vizuri sana pamoja na kwamba ni mara yao ya kwanza kushiriki, pia timu yetu ya netiboli na timu za kamba wanawake na wanaume zipo vizuri pia,” amesema Bi. Debora.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ismail Abdallah amesema mwaka huu wanatarajia kutwaa ubingwa baada ya mwaka jana kumaliza katika nafasi ya tatu, na endapo dhamira yao ya kutwaa ubingwa ikashindikana basi watajitahidi washike nafasi ya pili.

Bw. Abdallah amesema mbali na mchezo huo wamejiandaa kushiriki mchezo wa mpira wa netiboli, kuvuta kamba wanawake na michezo ya jadi.

Halikadhalika, Katibu Mkuu wa timu ya RAS Mbeya, Bi. Lilian Gombanila amesema mwaka huu wamekuja kivingine baada kupata baraka zote kutoka kwa mwajiri wao Katibu Tawala mkoa wa Mbeya aliyefanikisha pakubwa kushiriki kwenye michezo hii, hivyo wanauhakika wa kutwaa ubingwa wa mpira wa miguu.

“Hii michezo inatusaidia sana watumishi kwa kufahamiana na kutukumbusha kutekeleza kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma na kufanya kazi kwa bidii na kuimarisha afya ya mwili na akili, na tunaendelea kumuomba Mwenyezimungu kulilinda shirikisho hili liendelee zaidi na zaidi ili tuendelee kushiriki kwa wingi na tunashukuru Rais wetu kwa kuendelea kuipa kipaumbele michezo hii,” amesema Bi.Lilian.

Hatahivyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Utumishi SC, Bw. Charles Shija amesema wamekuja kutetea ubingwa wao wa soka na kutwaa ubingwa wa michezo mingine ikiwemo mpira wa netiboli, riadha, mbio za baiskeli na michezo ya jadi, ambayo mwaka jana hawakuweza kutwaa ubingwa.

“Kikosi chetu kimejiandaa vizuri na kimekamilika na ni wachezaji kama watatu hivi hawajafika ila watafika kwa ndege usiku huu, na tunamshukuru sana Katibu Mkuu Bw. Juma Mkomi, na Menejimenti yote ya Utumishi na Mkurugenzi wa Utawala na Wasaidizi wake wote na ofisi nzima kwa kuiombea timu yetu na tumefika Mwanza salama tayari kuanza michezo yetu,” amesema Bw. Shija.

Michezo ya 39 yenye kaulimbiu ya “Michezo kwa Watumishi Huongeza Tija Kazini: Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu” inatarajia kushirikisha takribani klabu zaidi ya 60, ambavyo vitaumana kwenye michezo ya mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, mbio za baiskeli, riadha, bao, karata, draft na vishale (darts), ambapo itachezwa kwenye viwanja vya CCM Kirumba, Nyamagana, Nsumba, Mabatini, Sabasaba na shule ya sekodari ya wavulana ya Bwiru





No comments:

Post a Comment