Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimishwa jijini Antananarivo Agosti 17, 2025, huku viongozi hao wakihimizana, umoja, mshikamano na ushirikiano kama njia ya msingi ya kujikwamua kiuchumi na kukabiliana na changamoto zinazoibuka kila siku ulimwenguni.
Katika mkutano huo, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, na kama ilivyo ada, mwenyeji wa mkutano huo, Madagascar alikabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka Zimbabwe.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi 9 ambapo Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, mwenyekiti aliyopekea kijiti, Katibu Mtendaji wa SADC na wakuu wa nchi wanne wa Botswana, Namibia, Msumbiji na Mauritius kutokana na kushiriki kwao kwa mara ya kwanza kama wakuu wa nchi walipata fursa ya kuhutubia mkutano huo.
Hotuba za viongozi hao ziligusia maeneo makubwa manne ambayo ni amani na usalama, ujenzi wa miundombinu, uchumi, demokrasia na mtangamano.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa alisema kuwa hali ya kisiasa katika kanda ni ya kuridhisha isipokuwa mashariki mwa DRC. Alisema jitihada zinazoendelea zinahitaji umoja na mshikamano na dhamira ya dhati kuumaliza mgogoro huo. Alisisitiza umuhimu wa migogoro inayoibuka Afrika itatuliwe na waafrika wenyewe na kama kuna msaada kutoka nje ya Afrika, basi msaada huo utambulike kama ziada tu.
Kwa upande wa uchumi, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuendeleza viwanda, kilimo, biashara na uongezaji wa thamani wa malighafi. Walisema maeneo hayo yakiendelezwa vizuri yatakuza uchumi, yatazalisha ajira na kipato kwa watu wengi hasa vijana na wanawake. Rais wa Botswana, Mhe. Duma Boko alisema biashara baina ya nchi za Afrika ni njia muhimu ya kujikwamua kiuchumi.
Kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara reli, maji, nishati na TEHAMA, ilielezwa kuwa ni roho ya kuharakisha maendeleo na mtangamano, na nchi zilitakiwa kutafuta fedha ya kugharamia miradi ya miundombinu iliyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kikanda 2030 na kuridhia itifaki ya kuanzisha mfuko wa kikanda wa maendeleo ambapo hadi sasa nchi 9, Tanzania ikiwemo zimesaini itifaki hiyo.
Kwa upande wa demokrasia, ulitolewa wito kwa nchi zote kuimarisha taasisi zinazosimamia masuala ya kukuza demokrasia na kuimarisha Misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya SADC kwa lengo la kuhakikisha nchi wanachama zinaendesha chaguzi za huru, haki na wazi.
Kuhusu kuimarisha mtangamano, nchi wanachama zilihimizwa kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma muingiliano wa watu baina ya nchi na nchi na ufanyaji wa biashara. Nchi wanachama zilihimizwa kuondoa sharti la viza na vikwazo visivyo vya kiforodha baina yao ili kukuza na kuimarisha mtangamano kwa lengo la kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment