
Serikali imepanga kuanzisha utaratibu wa kukopesha majiko ya umeme kwa bei ya ruzuku kwa wateja wapya wa umeme, ambapo malipo yake yatafanyika kidogokidogo kupitia ankara za kila mwezi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alitangaza hatua hiyo Agosti 22, 2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya ugawaji wa majiko ya nishati safi kwa watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“Kila mteja mpya wa umeme ataunganishwa na jiko la umeme ambalo atalipia kwa bei ya ruzuku na gharama hiyo atalipa kidogokidogo kupitia bili ya umeme,” alisema Dk. Biteko.
Aliongeza kuwa lengo ni kuhakikisha taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinakuwa mfano wa kwanza kwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.
Akitoa takwimu, Dk. Biteko alisema tafiti zinaonyesha kuwa kupika kwa kuni kunachukua hadi saa saba, huku kwa jiko la umeme ni saa moja pekee, jambo linalopunguza gharama, kulinda mazingira na afya za watumiaji.
“Kwa mfano, kupika kwa kutumia jiko la umeme hutumia uniti moja tu ya umeme yenye gharama ya shilingi 354, ambayo ni nafuu zaidi ya kuni na mkaa,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesm Mramba, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwamba ifikapo mwaka 2024 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Watumiaji wa nishati safi wameongezeka kutoka asilimia 6.9 hadi 20.3 kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan. Kwa kasi hii, asilimia 80 inaweza kufikiwa hata kabla ya mwaka 2024,” alisema Mramba.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Meja Jenerali mstaafu Jacob Kingu, alizitaka taasisi zote chini ya wizara kuhakikisha watumishi wake wote wanapatiwa majiko hayo ili kuwa chachu ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy, alisema jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi zinaendelea, ikiwemo kufunga majiko katika Jeshi na shule mbalimbali.
“Mwaka huu tumepanga kusambaza majiko ya nishati safi katika shule 53 kwa watumishi 2,192 kwa kuwapatia mitungi ya LPG. Aidha, tumeweka bajeti ya Sh bilioni 20 kwa ajili ya taasisi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia,” alisema Saidy.




No comments:
Post a Comment