Na Mwandishi Wetu-Manyara
WAZIRI wa Maliasili na Utalii wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka (LATF Governing Council), Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ameongoza kikao cha ngazi ya juu cha kuamua hatma ya uongozi wa Mkurugenzi wa LATF, Edward Phiri, ambaye mkataba wake ulikuwa umemalizika.
Kikao hicho cha 'Ministerial Bureau', kilichofanyika leo, Agosti 15, 2025, kwa njia ya mtandao kimejumuisha viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Maliasili wa Zambia, Mhe. Rodney Sikumba pamoja na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Kutoka Tanzania wamehudhuria Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, CP Benedict Wakulyamba, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Alexander Lobora na Bw. Ezekiel Goboro. Pia, Kenya iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kwa niaba ya viongozi wa wizara hiyo.
Katika kikao hicho, nchi wanachama wamekubaliana kwa pamoja kumpa Phiri mkataba mpya wa miaka mitatu kuendelea kuiongoza sekretarieti ya LATF, kutokana na utendaji wake mzuri uliotambulika na kuthaminiwa na wanachama wote.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Chana amesisitiza umuhimu wa kuwa na utaratibu thabiti wa urithishanaji wa madaraka ndani ya LATF ili kuhakikisha uwiano wa kiuongozi kati ya nchi wanachama.
"Sekretarieti iandae rasimu ya mapendekezo ya ukomo wa muda wa Mkurugenzi wa LATF ili kutoa nafasi kwa nchi wanachama kushiriki kikamilifu katika uongozi," ameeleza Mhe. Chana.
Kwa upande wake, Phiri amewashukuru viongozi wa nchi wanachama kwa kuendelea kumuamini, akiahidi kuendelea kulitumikia Baraza hilo kwa weledi, uadilifu na kujituma kwa maslahi ya pamoja.
Baraza la Ministerial Bureau lina mamlaka ya kufanya maamuzi kwa niaba ya nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka. Kwa sasa, Tanzania inashikilia nafasi ya Urais, Congo Brazzaville ni Makamu wa Rais, huku Zambia ikiwa ni Rapporteur wa kikao hicho.
No comments:
Post a Comment