ZAIDI YA WAGENI 140 KUTOKA MATAIFA MBALIMBALI WATEMBELEA HIFADHI YA KILWA KISIWANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 5, 2025

ZAIDI YA WAGENI 140 KUTOKA MATAIFA MBALIMBALI WATEMBELEA HIFADHI YA KILWA KISIWANI



Na Mwandishi Wetu, Lindi


Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara wilayani Kilwa imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo tarehe 31 Oktoba 2025 ilipokea jumla ya watalii 147 kutoka mataifa mbalimbali duniani waliowasili hifadhini humo kwa kutumia meli ya kifahari iitwayo SH Diana, kwa lengo la kutalii na kujionea vivutio vya kihistoria vilivyopo katika eneo hilo.

Watalii hao walitoka katika nchi 13 zikiwemo Ufaransa, Australia, Ubelgiji, Canada, Uingereza, Uswisi, Ujerumani, Cyprus, New Zealand, Marekani, Urusi, Uturuki na Ukraine. Ziara hiyo iliratibiwa na kampuni za Savannah Tours Ltd kwa kushirikiana na Black Willow Safaris.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya watalii hao, Kamanda wa Hifadhi hiyo, Mhifadhi Mwandamizi Kelvin Stanslaus, alisema ujio wa wageni hao ni ishara njema kwa ukuaji wa utalii wa urithi nchini, hasa ikizingatiwa umuhimu wa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kama maeneo yaliyosajiliwa na UNESCO kuwa Urithi wa Dunia tangu mwaka 1981.

“Tunayo furaha kubwa kuona wageni kutoka pande mbalimbali za dunia wakija kujionea historia adhimu ya Kilwa, ambayo ni alama muhimu ya biashara ya kimataifa ya karne za kati kati ya Afrika Mashariki na Dunia,” alisema Afisa huyo.

Aidha, wageni hao walipata fursa ya kutembelea majengo ya kihistoria ikiwemo Msikiti Mkongwe, na Kasri la Sultani, ambapo walivutiwa na usanifu wa majengo ya mawe pamoja na simulizi za kihistoria zinazoambatana na maeneo hayo kutoka Kwa Maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA waliobobea na kutopea katika masuala ya malikale.

Kwa mujibu wa TAWA ambayo ndiyo wasimamizi wa hifadhi hiyo, ujio wa meli hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuimarisha utalii wa urithi, hususan katika maeneo ya bahari, malikale na visiwa vyenye thamani ya kihistoria.














No comments:

Post a Comment