
NA. MWANDISHI WETU- SHINYANGA
Waziri wa nchi Ofisi ya waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge William Lukuvi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa viongozi wa Serikali waliopo maeneo ya ajali ya mgodini kushiriki taratibu zote za mazishi kwa walifariki ajali ya mgodini na kuwakilisha rambirambi zake kwa wahusika huku akisihii kuendelea kuratibu vyema shughuli ya uokoaji inayoendelea.
Ameyasema hayo wakati wa kikao na viongozi pamoja na ndugu wa waathirika wa ajali ya mgodini katika eneo la tukio la ajali ya mgodi unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi katika machimbo ya Nyandolwa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
“Rais Samia kaniagiza kuwafikishia salamu za pole na rambirambi pia kanituma kuleta maagizo kwa viongozi wa serikali waliopo eneo hili kuhakikisha wanahudhuria misiba yote ya watu waliopoteza maisha katika ajali hii na kuwakilisha rambirambi alizotoa katika familia hizo” amesema Lukuvi.
Agosti 16, 2025 Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk. Kalekwa Kasanga kufanya utaratibu wa kuweka ofisi ya muda ya mtendaji wa kijiji katika eneo la tukio la ajali ambayo itatumika kuwasajili wageni waliokuja kusubiri ndugu zao kwa ajili ya kuhudumiwa na serikali.
Mnamo Agosti 18, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita alitoa maelekezo kwa familia zilizokuja kusubiri ndugu zao, kuchagua wawakilishi wawili au watatu ambao watabaki ili iwe rahisi kwa serikali kuhudumia familia hizo na kupewa mahitaji muhimu.
Aidha, Agosti 11, mwaka huu watu 25 walifukiwa na Mgodi wa Kikundi cha Wachapakazi katika Machimbo ya Nyandolwa na hadi sasa watu 11 wametolewa huku watatu wakiwa hai na nane wakiwa wamefariki, na juhudi za kuendelea kuwatoa wengine 14 zinaendelea kwa kasi kwa kutumia mashine za utambuzi wa ardhini kujua maeneo waliopo.






No comments:
Post a Comment