Na Carlos Claudio, Dodoma.
WIZARA ya Katiba na Sheria imebainisha kuwa zaidi ya wananchi milioni 4 nchini wamefikiwa na huduma za msaada wa kisheria kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 300 yaliyosajiliwa rasmi kutoa huduma hiyo.
Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Bi. Easter Msambazi, ametoa taarifa hiyo leo Agosti 12, 2025 jijini Dodoma, wakati akichangia mada katika kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs).
Bi. Msambazi, ambaye pia ni Msajili wa Mashirika ya Msaada wa Kisheria nchini, amesema huduma hizo zimewezesha kutatuliwa migogoro zaidi ya 26,000, ikiwemo migogoro ya papo kwa papo ambayo imepatiwa ufumbuzi mara moja.
Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa mashirika hayo, sambamba na kampeni na mikakati inayoendeshwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kumeongeza kasi ya utoaji huduma za msaada wa kisheria, hasa katika maeneo ya vijijini.
“Tunapongeza mashirika haya kwa mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, lakini pia tunasisitiza umuhimu wa kuwa na vyanzo vya ndani vya rasilimali fedha ili kuepuka utegemezi kwa wadau wa maendeleo,” alisema Bi. Msambazi.
Katika kongamano hilo, wadau walihimizwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na serikali na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata haki zao kwa wakati.
No comments:
Post a Comment