AQRB YASISITIZA UJENZI WA MAJENGO MAKUBWA USHIRIKISHE WATAALAMU KWA ASILIMIA 100 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 16, 2025

AQRB YASISITIZA UJENZI WA MAJENGO MAKUBWA USHIRIKISHE WATAALAMU KWA ASILIMIA 100


Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) , Arch. Dkt. Daniel Matondo,akizungumza na waandishi wa habari Septemba 16,2025 jijini Dodoma, kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Bodi hiyo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 15 hadi 17, 2025 jijini Arusha.


NA OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) imewataka wawekezaji na wananchi kwa ujumla kufuata sheria na taratibu za ujenzi kwa kutumia wataalamu waliosajiliwa na mamlaka husika, ili kukabiliana na tatizo la kuporomoka kwa majengo makubwa nchini.

Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, Arch. Dkt. Daniel Matondo, ameyasema hayo Septemba 16,2025 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Bodi hiyo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 15 hadi 17, 2025 jijini Arusha.

Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria, kila mtu anayejenga majengo makubwa au ya umma ikiwamo makanisa na misikiti, anatakiwa kushirikisha wataalamu waliosajiliwa katika hatua zote za ujenzi kwa asilimia 100.

“Watu wote wanaojenga majengo yanayoguswa na sheria hii wanapaswa kushirikisha wataalamu waliosajiliwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwamo majengo kuporomoka na kuleta maafa katika jamii,” amesema Dkt. Matondo.

Kuhusu mkutano huo, alisema utawakutanisha wadau na wataalamu wa sekta ya ujenzi kujadili changamoto na fursa katika maeneo mbalimbali. Mada zitakazojadiliwa zitahusu miongoni mwa mengine:
Taratibu za vibali na usajili wa kisheria.

Usalama mahali pa kazi na uzingatiaji wa usalama wa moto katika usanifu wa majengo, uendelevu wa mazingira na tathmini za athari za kimazingira, Maadili ya kitaaluma na masharti ya Usajili, hatari na wajibu wa kisheria katika miradi ya ujenzi na zana za ufuatiliaji na uwasilishaji wa taarifa za uzingatiaji.

Amebainisha kuwa kupitia mijadala hiyo, mkutano utasaidia kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za udhibiti, kujenga uwezo wa wataalamu, kuimarisha ufanisi wa utekelezaji wa sheria na miongozo ya ujenzi, na hatimaye kukuza miradi bora, salama na endelevu kwa manufaa ya taifa.

Dkt. Matondo aliongeza kuwa mkutano huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Blueprint for Regulatory Reforms (2020) inayosisitiza ushirikiano wa taasisi na kujenga uwezo wa kitaalamu ili kuboresha udhibiti katika sekta ya ujenzi.

Kwa mujibu wake, taasisi za udhibiti zitakazoshiriki ni pamoja na AQRB, ERB, CRB, OSHA, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, EWURA, NEMC na TAMISEMI, ambazo zitaandaa na kuwasilisha mada au tafiti kulingana na majukumu yao.

Aidha, mbali na taasisi za ndani, AQRB pia imealika wageni kutoka nje ya Tanzania wakiwemo wataalamu wa usanifu majengo, ukadiriaji majenzi, pamoja na vyama na bodi za kitaaluma za kimataifa, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) , Arch. Dkt. Daniel Matondo,akizungumza na waandishi wa habari Septemba 16,2025 jijini Dodoma, kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Bodi hiyo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 15 hadi 17, 2025 jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment