DKT. ABBASI AKABIDHI VIFAA VYA KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 28, 2025

DKT. ABBASI AKABIDHI VIFAA VYA KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU


Na Mwandishi Wetu- Goha,Korogwe


Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amekabidhi mabomu baridi mia nne (400), pikipiki mbili na ndegenyuki (drone) moja kwa kituo cha askari uhifadhi Goha wilayani Korogwe mkoani Tanga kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.

Akikabidhi vifaa hivyo leo Septemba 28, 2025 Dkt. Abbasi amesema hiyo ni hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa kudhibiti mwingiliano wa binadamu na wanyamapori ili kupunguza madhara kwa jamii.

“Mnafahamu nchi nzima kuna maeneo mengi yenye changamoto za muingiliano wa wanyama wakali na waharibifu ambao wanaharibu mazao, mimea mingine na wanashambulia binadamu hivyo kama Wizara tuna mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na changamoto hiyo” amesisitiza Dkt. Abbasi.

Amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo kisayansi na kioparesheni ikiwa ni pamoja na kuchimba mabwawa ikiwepo ya Wilaya ya Same, kutumia helikopta kuwarudisha wanyama hifadhini na kutumia ndegenyuki ambazo zilishakabidhiwa katika kituo hicho na kote nchini. 

“Tunaamini vifaa hivi vitaongeza ufanisi wa kuwafukuza hasa wanyama wakali kama tembo ili wananchi wetu wazidi kuwa salama na waweze kufanya shughuli zao kwa amani” amefafanua Dkt. Abbasi. 

Dkt. Abbasi amewaomba Wananchi kuzingatia maelekezo wanayopewa wakati wa kukabiliana na changamoto hiyo na pia kutoa taarifa kwa askari kupitia namba maalum za askari inayotumika katika wilaya zote ili kuepusha taharuki.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Bw. Emmanuel Moirana ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kukabidhi vifaa hivyo na kusisitiza kuwa vitaenda kutatua changamoto ya Wanyama wakali na waharibifu kwa kuwa ni kubwa katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa lengo ni kuboresha ufukuzaji wa tembo, kuongeza upataji wa taarifa sahihi tembo walipo na kubaini chanzo cha tatizo hivyo amewaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kupunguza madhara ya tembo.

Makabidhiano hayo ni muendelezo wa utekelezaji wa mkakati wa kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu nchini.

No comments:

Post a Comment