Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kutoa fursa za ajira kwa Vijana ikiwa atachaguliwa kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo, akiahidi kuja na kongani ya Viwanda kwenye Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida ili kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa eneo hilo.
Dkt. Samia anayepeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Urais 2025, ameyaeleza hayo leo Jumanne Septemba 07, 2025 wakati akizungumza na maelfu ya wananchi Wilayani Ikungi Mkoani Singida, akisema katika kipindi chake cha awamu ya kwanza alifanikiwa kupeleka kiwanda kimoja kikubwa Wilayani humo na hivyo kutoa fursa ya ajira.
Dkt. Samia pia amebainisha mafanikio makubwa Wilayani humo katika ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji Mkoani humo, ikiwemo barabara ya Singida- Sepuka- Ndago- Kizaga (Kilomita 77) akisema kwa miaka mingine mitano wataendelea kuboresha huduma ya miundombinu.
"Mahitaji bado ni mengi tutajenga barabara ya Misugaa-Ntutu lakini pia Iglasone-Mkenene mpaka Iyumbo lakini pia Mnang'aa na Mwasutiyanga kwa kiwango cha changarawe pamoja na ujenzi wa barabara ya Ikungi- Londoni- Solya kwa kiwango cha lami. Tutaendeleza pia barabara za katikati ya Mji sambamba na kuweka taa za barabarani eneo la Puma." Amesema Dkt. Samia.
No comments:
Post a Comment