
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Septemba 10, 2025 anaendelea na Kampeni zake Mkoani Singida, akitarajiwa katika siku yake hii ya pili kuwa na Mkutano mkubwa eneo la Misigiri, Wilayani Iramba na kisha kuelekea Mkoani Tabora.
Jana Jumanne akiwa Singida Mjini, Manyoni na Ikungi, Mgombea Urais huyo amesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa Tanzania kwa kulinda na kuendeleza utu wa Kila Mwananchi kupitia utoaji wa huduma bora za Kijamii ikiwemo huduma za afya, elimu, Maji pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi kupitia fursa mbalimbali sambamba na uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Kulingana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025/30, Chama hicho kwa Wilaya ya Iramba pamoja na mambo mengine kimeahidi kujenga chuo cha mafunzo ya ufundi stadi VETA, Ujenzi wa daraja lenye urefu wa Mita 120 Mto Nzalala sambamba na kujenga barabara ya sabasaba- Sapuka- Ndago- Kizaga kwa kiwango cha lami na barabara ya Ulemo- Gumanga na Nduguti- Nkingu kwa kiwango cha lami.

"CCM inatambua matarajio makubwa waliyonayo wananchi wa Singida, Niwathibitishie kwamba Mimi binafsi pamoja na Chama Changu tuna uwezo, uzoefu na ari ya kutimiza matarajio yenu. Tunadhamiria kuweka mkazo katika uimarishaji wa nyanja zote za maisha ya binadamu ikiwemo elimu, ajira, afya, maji, kilimo, ufugaji na uhifadhi wa mazingira. Kwa pamoja tutaendeleza mafanikio tuliyoyapata na kufanya mengine mapya ili kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuboresha maisha ya wananchi wa Singida na Watanzania." Alikaririwa Dkt. Samia.
Katika awamu yake ya kwanza ya Uongozi wa serikali ya awamu ya sita, Serikali ya Rais Samia ilifanikisha ujenzi wa vituo 3 vya afya vya Mtoa, Mwandegembe na Irungu, ujenzi wa shule mpya ya amali Wilayani Iramba, shule ya sekondari Mbelekese pamoja na ujenzi wa tenki la maji Kizonzo lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 300, 000 kando ya uanzishwaji wa soko la dhahabu lililoanzishwa ndani ya Wilaya hiyo, miongoni mwa Wilaya zinazounda Mkoa wa Singida

No comments:
Post a Comment