Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa kikao cha Waratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 15–19 Septemba 2025 ambacho kimeshirikisha taasisi 22 kwa lengo la kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeshiriki kama moja ya taasisi nufaika ya mradi huu.
Akifungua kikao hicho Mratibu wa Mradi wa HEET Kitaifa, Dkt. Kenneth Hosea amewataka waratibu hao kutumia kikao hicho kubadilishana uzoefu katika kuboresha utekelezaji wa mradi huo, ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 74.3 hali inayoonesha kasi nzuri ya shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Mratibu wa Mradi HEET IAA, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa HEET IAA, Bw. Emmanuel Pallangyo amesema, IAA kupitia mradi huu IAA inaendelea na ujenzi wa majengo ya TEHAMA, taaluma, utawala, maktaba na maabara ya kompyuta katika kampasi za Songea, Babati na Arusha ambayo yatachangia kuboresha mazingira ya ufundishaji, ujifunzaji na kuongeza udahili wa wanafunzi.
Aidha, Pallangyo amesema ujenzi wa majengo hayo umezingatia miundombinu wezeshi kwa watu wenye mahitaji maalum, huku akibainisha kuwa jumla ya wananchi 1055 wamepata ajira za muda katika ujenzi unaoendelea ikiwemo ujenzi, utoaji wa huduma za chakula na ufundi mbalimbali, ambazo zinawasaidia kujipatia kipato kwa ajili ya kujikimu kimaisha.
Pamoja na ujenzi wa miundombinu, Pallangyo amesema mradi wa HEET umewezesha IAA kuhuisha jumla ya mitaala 08 ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira, kutoa mafunzo ( Shahada ya Uzamivu) kwa watumishi 22 , kuimarisha ushirikiano wa kisekta katika ya Chuo na wadau ikiwemo sekta binafsi na kuongeza uelewa wa masuala ya jinsia na elimu jumuishi katika utoaji wa elimu.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mradi huu imetenga jumla ya shilingi bilioni 48 kwa ajili ya IAA ili kuwezesha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi, kuimarisha ushirikiano wa kisekta na kuimarisha masuala ya jinsia na elimu jumuishi.
No comments:
Post a Comment