
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, amesisitiza kuwa Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora itakuwa kitovu cha maendeleo kupitia miradi mikubwa ya afya, elimu, maji, kilimo, mifugo na miundombinu katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwa atachaguliwa kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2025 leo Septemba 11, 2025 Wilayani Kaliua, Dkt. Samia amebainisha kwamba ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na zahanati nane tayari umekamilika, huku huduma za afya zikiboresha hali ya maisha ya wananchi.
Aidha amesema miradi ya elimu inaendelea kuimarika kwa kutekeleza ujenzi wa shule maalumu za wasichana za Mkoa wa Tabora, vyumba vipya vya madarasa, bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu, na maabara katika Shule Sekondari Isike.
Dkt. Samia ameongeza kuwa miradi ya maji safi na salama inaendelea kupanuliwa ikiwemo upanuzi wa miradi ya maji na uchimbaji wa visima vipya. Katika sekta ya kilimo, kuimarika kwa upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kutasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, huku miradi ya skimu za umwagiliaji ikijenga bwawa na skimu katika maeneo kama Kona 4, Igombe, Mnange, Limbula na Igwisi. Aidha, mifugo pia itapata huduma bora kutokana na maboresho ya miundombinu.
Akizungumzia miundombinu, Dkt. Samia ameahidi kuendeleza barabara za lami na changarawe, kusimika taa za barabarani, kuimarisha huduma za umeme na kujenga vibanda vya biashara, yote kwa lengo la kuinua kipato na maisha ya wananchi.


No comments:
Post a Comment