
BODI ya Wakurugenzi ya Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) imetoa wito kwa taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa mafuta nchini kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha taratibu za upakiaji na upakuaji mafuta zinafuatwa kwa kuzingatia usalama wa watu na uhifadhi wa mazingira.
Wajumbe wa Bodi hiyo wametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua huduma za shehena za mafuta katika Bandari za Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma. Walisema kuwa upakiaji wa mafuta bila kutumia mifumo rasmi ni hatari, kwa kuwa unaweza kuharibu mazingira na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya PBPA, Dkt. Lutengeno Mwakahesya, alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha miundombinu yote ya kusafirisha mafuta inazingatia viwango vya usalama na heshima kwa mazingira.
“Kushusha mafuta moja kwa moja kutoka kwenye malori hadi melini bila kutumia terminal ni hatari. Tunashauri TPA iangalie uwezekano wa kujenga matenki mapya ya kuhifadhia mafuta au kuboresha yaliyopo kupitia maboresho yanayoendelea ya Bandari ya Kigoma,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vyema TPA ikaweka utaratibu wa bei sawa (equal pricing) kwa shughuli zote za kushusha na kusafirisha mafuta kupitia Kigoma ili kurahisisha matumizi ya terminal, kupunguza gharama kwa wadau na kuongeza usalama wa shughuli hizo.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Kigoma, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula, alisema kwa sasa bandari hiyo inatumia mfumo wa dipping system, huku maandalizi yakiendelea ili kuanza kutumia flow meter system yenye ufanisi zaidi.
Mabula alisema biashara ya mafuta katika bandari hiyo imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka. “Kwa mfano, mapokezi ya mafuta yameongezeka kutoka tani 32,826 mwaka 2023 hadi tani 52,367 mwaka 2024. Hii inaonyesha jinsi uhitaji wa huduma unavyoongezeka,” alisema. Alifafanua kuwa mafuta hayo huhudumiwa kupitia cargo terminal na kusafirishwa kwa meli ya Sangara kwenda nchi jirani za Burundi na Congo. TPA, alisema, imejipanga kuhakikisha uhitaji unaoongezeka unakidhiwa kwa wakati.
Mabula aliongeza kuwa wakati wa upakiaji wa mafuta, taasisi za zimamoto huhakikisha zipo eneo la bandari kama hatua ya tahadhari ya kulinda usalama wa watu na mazingira. Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Bandari ya Kigoma, Mohamed Mnonda, alisema taasisi yake kwa kushirikiana na TPA, EWURA na wadau wengine inasimamia kwa karibu mizigo yote inayosafirishwa nje ya nchi kupitia Kigoma.
“TRA inahakikisha mizigo yote inapimwa na kusajiliwa ipasavyo ili kuepusha upotevu wa mapato ya Serikali na kulinda usahihi wa takwimu za biashara,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya GBP Tanzania Bw. Rashid Seif aliomba Serikali kuruhusu tena biashara ya mafuta ya kusafirisha nje (export) kupitia bandari za Ziwa Tanganyika. Alisema kufungwa kwa mfumo huo kumesababisha makampuni mengi kufunga depoti zao, lakini kama mfumo huo ukifunguliwa upya, makampuni yatatumia tena matenki yao, jambo litakaloongeza mapato ya Serikali na kuchochea ajira kwa wananchi wa Kigoma.
Serikali kwa sasa inaendelea na maboresho ya Bandari ya Kigoma na zingine za Ziwa Tanganyika, lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kubwa za mafuta na bidhaa nyingine. Maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania katika ukanda wa Maziwa Makuu na kusaidia kukuza biashara na usafirishaji kwenda nchi jirani za Burundi, Congo na Zambia.







No comments:
Post a Comment