SEKTA YA MADINI YAIMARISHA KILIMO KUPITIA VIWANDA VYA MBOLEA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 11, 2025

SEKTA YA MADINI YAIMARISHA KILIMO KUPITIA VIWANDA VYA MBOLEA




Na Mwandishi Wetu, Tanga


Sekta ya Madini inaendelea kuwa mhimili wa maendeleo ya viwanda na kilimo nchini, hususan kupitia madini ya viwandani kama dolomite, chokaa (limestone), gypsum (jasi) na phosphate, hatua inayochangia ukuaji wa Sekta ya Viwanda nchini pamoja na namna Sekta ya Madini inavyosaidia kuunganisha Sekta nyingine kama viwanda, kilimo na ujenzi.

Akizungumza na Madini Diary, Septemba 10, 2025, jijini Tanga, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanga Mining Limited, Rishit Lalseta, alisema madini ya viwandani kama dolomite yamekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza viwanda vya mbolea na hatimaye sekta ya kilimo kwa ujumla.

“Dolomite ni nyenzo muhimu sana kwenye utengenezaji wa mbolea. Husaidia kuongeza kalsiamu na magnesiamu kwenye udongo, kurekebisha asidi na kufanya mazao kukua kwa afya na kutoa mavuno bora. Kwa maana hiyo, kilimo kinapewa nguvu ya ziada na wakulima kunufaika zaidi,” alisema Lalseta.

Kwa mujibu wa Lalseta, hatua hii ni kielelezo cha namna sekta ya madini inavyoweza kuunganisha viwanda na kilimo ili kufanikisha ajenda ya taifa ya uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu.

“Soko la mbolea ni kubwa sana ndani ya nchi, kwasababu mahitaji bado ni makubwa sana, kwa sasa soko letu lipo ndani ya nchi, tunafikiria pia kwa siku za usoni kutafuta masoko ya kimataifa ili pia tuweze kuisaidia nchi kuleta fedha za kigeni kupitia bidhaa zinatengenezwa na kiwanda chetu ndani ya nchi” aliongeza Lalseta.

Ameeleza kuwa, kupitia matumizi ya mbolea yenye virutubisho vinavyotokana na dolomite, wakulima wameweza kuongeza tija na ubora wa mazao yao, hali ambayo inachangia kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza pato la taifa.

Aidha, Lalseta alibainisha kuwa kuanzishwa kwa kiwanda mnamo hicho mwaka 2014, kumeongeza ajira kwa wananchi wa Tanga na maeneo jirani, pamoja na mapato kwa Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Laurent Bujashi, alelezea hatua hiyo kuwa ni mfano mzuri wa namna Sekta ya Madini nchini inavyoweza kuchochea maendeleo ya viwanda, kilimo na ujenzi kwa pamoja.

“Tunaposhuhudia madini ya viwandani kama dolomite yakitumika kuongeza thamani kwenye viwanda vya mbolea, maana yake tunaleta suluhisho kwa changamoto za kilimo na usalama wa chakula nchini. Hii ni njia ya kuhakikisha madini yanawanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia sekta za kilimo, viwanda na ujenzi” alisema Mhandisi Bujashi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Bujashi, mchango wa madini ya viwandani katika Sekta za viwanda, kilimo na ujenzi ni kielelezo cha dhamira ya Serikali kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi.





No comments:

Post a Comment