
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Septemba 17, 2025 anarejea tena kwenye Ziara za Kampeni zake kuelekea uchaguzi Mkuu wa Jumatano ya Oktoba 29, 2025 na zamu hii ni Visiwani Zanzibar - akitarajiwa kuwa na Mikutano kwenye Wilaya za Kusini Unguja na Makunduchi Kusini Mashariki ya Unguja.
Dkt. Samia kufikia sasa tayari amekutana na wapigakura kwa kufanya Mikutano kadhaa ya kampeni kwenye Mikoa ya Dar Es Salaam, Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Singida, Tabora na Mkoa wa Kigoma, akinadi sera na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM kuelekea mwaka 2030 pamoja na kuorodhesha msururu wa mafanikio yaliyopatikana kwenye kipindi cha miaka minne na nusu ya serikali yake ya awamu ya sita.
Dkt. Samia katika siku zake 100 za awali ikiwa atapewa ridhaa na Watanzania hapo Oktoba 29, Ameahidi kuwa utawala wake katika kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, kwa kuanza na awamu ya majaribio pamoja na kugharamia matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo kwa magonjwa ya saratani, moyo, sukari, figo, mifupa na mishipa ya fahamu.
“Haya ndio magonjwa yenye gharama kubwa ambayo wananchi wasio na uwezo hushindwa kuzimudu na katika kuimarisha huduma za afya, serikali itaajiri wahudumu wa afya wapya 5,000 ndani ya siku 100, wakiwamo wauguzi na wakunga, ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto,” alisema.
Kwa upande wa sekta ya elimu, ameahidi kuja na mkakati kuwezesha mtoto kufikia darasa la tatu awe anajua kusoma, kuhesabu na kuandika bila shida.
Ameahidi pia kuajiri walimu 7,000 wa hisabati na sayansi. Ahadi nyingine ni kuzindua mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu ili kutangaza mahitaji ya kipaumbele na kuwawezesha wanafunzi wa VETA wanapotoka darasani wachukuliwe viwandani wafanye mazoezi.
Aidha Dkt. Samia amesema serikali yake itatenga Shilingi bilioni 200 ya mitaji ya wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na kuimarisha kampuni changa, akipanga pia kurasimisha sekta isiyo rasmi ili wajasiriamali wapate huduma wanazostahili.
Ametangaza kadhalika ujio wa programu maalumu ya mitaa au kongani za viwanda kwenye kila Wilaya kama sehemu ya jitihada za kuzalisha ajira na kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini na misitu sambamba na kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji ili Taifa kuwa na uhakika wa maji safi, salama na ya uhakika kwa shughuli za nyumbani, Kilimo, Mifugo na biashara.
No comments:
Post a Comment