TAKUKURU na Mahakama mabingwa wapya wa baiskeli SHIMIWI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 6, 2025

TAKUKURU na Mahakama mabingwa wapya wa baiskeli SHIMIWI



Na Mwandishi Wetu, Mwanza


WAKATI michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa nchini (SHIMIWI) ikitarajiwa kufunguliwa kesho tarehe 07 Septemba, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dotto Biteko, wachezaji wa timu za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na Mahakama leo wameibuka mabingwa wa mchezo wa mbio za baiskeli kwa wanawake na wanaume za kilometa 50 na 30 zilizoanzia eneo la Igoma karibu na Makaburi ya Mv Bukoba jijini Mwanza.

Kwa upande wa wanaume ambao walishindana kwenye mbio za Kilometa 50, ambazo zilianzia eneo hilo la Igoma na kugeuzia eneo la Nyanguge zikiwa ni Km 25 kwenda na kurudi walipoanzia, mchezaji Chacha Ikwabe wa TAKUKURU alimaliza mbio hizo za kilometa 50 kwa wanaume kwa kutumia muda wa saa 1:21.47.

Mshindi wa pili kwa wanaume ameshinda Bw. Salum Ndambwe wa Wizara ya Ujenzi aliyetumia muda wa saa 1:26.21 na mshindi wa tatu ni Bw. Hassan Ligoneko wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aliyemaliza kwa muda wa saa 1:27.02. Bw. Ligoneko ndiye alikuwa bingwa mtetezi.

Kwa upande wa wanawake ambao nao walianzia eneo la Igoma Makaburi ya Mv Bukoba kwa mbio za kilometa 30, zikiwa ni Km. 15 kwenda na kugeuzia eneo la Isangijo na kurudi walipoanzia, ubingwa umechukuliwa na Bi. Mwajabu Bwire wa Mahakama aliyetumia muda wa saa 1:06.35; akifuatiwa na aliyekuwa bingwa mtetezi Bi. Alavuya Mtalemwa wa Wizara ya Mambo ya Ndani aliyetumia saa 1:07.44 na watatu ameshika Bi. Donasia Tesha wa Wizara ya Fedha aliyetumia saa 1:12.34.

Bingwa wanawake, Bi. Mwajabu amesema ameshinda kutokana na hamasa za viongozi wake na pia kufanya mazoezi kwa bidii baada ya kushika nafasi ya pili kwenye michezo ya Kombe la Mei Mosi iliyofanyika mkoani Singida mwezi Aprili, 2025.

Lakini kwa mshindi wa pili ambaye amevuliwa Bi. Alavuya amempongeza mshindani wake kwa kuwa yupo vizuri, na amesema mashindano yalikuwa mazuri maana barabara ilikuwa ngumu yenye milima, mteremko na sehemu nyingine tambarare, na siri ya mafanikio yake ni kuwa na stamina na mazoezi anayofanya mara kwa mara.

Naye Bw. Ikwabe aliyeshika nafasi ya kwanza kwa wanaume amesema anaishukuru taasisi yake ya TAKUKURU kwa kufanikisha ushindi ikiwa ni pamoja na kuruhusu kufanya mazoezi ya mara kwa mara na pia kumnunulia baiskeli ya kisasa kabisa.

Naye Bw. Salumu amesema ushindi huu umempa hamasa zaidi na morali ya kufanya kazi pindi atakaporejea mahala pake pa kazi Jijini Dodoma; huku mshindi wa tatu kwa wanaume ambaye amewahi kuwa bingwa miaka mitatu mfululizo, Bw. Ligoneko amesema pamoja na kushika nafasi hiyo amejivunia wanafunzi wake vijana wenye umri mdogo aliokuwa akiwafundisha mara kwa mara kumshinda kwa kushika nafasi ya kwanza na ya pili. Ila ameushukuru uongozi mzima wa taasisi yake kwa kufanikisha maandalizi yake, anaamini mchezo wa baiskeli kwenye SHIMIWI unaendelea kukua kwa kuwa na vijana zaidi.

Hatahivyo, ametoa wito kwa taasisi, wizara na wakala za serikali kuiga mfano wa Ofisi yake kwa kutenga siku maalum za kufanya mazoezi kwa watumishi wao ili kuwajengea afya njema, wao wanafanya mazoezi kwa kila wiki siku za Jumanne na Alhamis kuanzia saa 10 jioni.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Bw. Alex Temba ameushukuru uongozi mzima wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na polisi kwa kupata huduma bora za ulinzi kwa muda wote wa mbio za baiskeli na hakuna mchezaji aliyepata madhara katika mchezo huo.

Amesema lengo la mashindano haya ni kujenga umoja na ushirikiano baina ya watumishi wa umma ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi kwa haraka na kwa wakati.








No comments:

Post a Comment