
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza adhma yake ya kuendelea kuijenga Tanzania yenye uchumi Jumuishi na ustawi kwa wote ikiwa atachaguliwa tena kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo, akitaja nia yake pia ya kuendelea kuimarisha Vyama vya ushirika na ushirika nchini ili kuwafanya wakulima kufaidi nguvu na jitihada zao katika Kilimo.
Mbele ya maelfu ya wananchi wa Mji wa Iringa leo Jumapili Septemba 07, 2025 kwenye uwanja wa michezo Samora Mkoani Iringa. Dkt. Samia ambaye amehitimisha ziara yake ya siku mbili Mkoani humo kwaajili ya kujinadi kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Dkt. Samia ameeleza kuwa katika kutekeleza hilo, amejipanga pia kuhimiza matumizi ya TEHAMA kwenye Sekta za kilimo nchini ikiwemo kwenye Ushirika ili kuendana na mahitaji halisi yaliyopo duniani.
Dkt. Samia amebainisha kuwa ataendelea pia kulea na kukuza vyama vya ushirika nchini ili viweze kusimama vyenyewe, kuwa na uwezo wa kutafuta mikopo, kusambaza pembejeo kwa wanachama na baadae kununua mazao, kutafuta masoko ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na uwezo wa kujenga maghala ya kuhifadhia mazao ya kilimo.
"Nataka niwahakikishie kwamba tumejipanga vyema kuvilea vyama vya ushirika na ushirika ndani ya nchi yetu na lengo ni kumuwezesha mkulima kufaidi nguvu na jasho lake na huku ndiko kumuinua Mkulima. Niwaambie pia kwamba la muhimu katika vyama vya ushirika ambalo tunalifanyia kazi ni kuhakikisha tuna watu mahiri kwenye kuelewa kuendesha ushirika lakini pia matumizi ya tehama ili kuongeza uwazi kwenye mapato na matumizi ya ushirika, huko ndiko kwenye kuleta vurugu mpaka ushirika unavunjika." Amesisitiza Dkt. Samia.
Akizungumzia jitihada ambazo tayari zimechukuliwa katika awamu yake ya kwanza Dkt. Samia amesema serikali yake ilichukua hatua kadhaa za makusudi ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya ushirika nchini pamoja na kuimarisha usimamizi wa Ushirika kupitia Tume ya maendeleo ya ushirika ili kuwezesha Vyama vya ushirika kupata mahitaji na mitaji nafuu katika kuwawezesha kujitegemea na kujiendesha.





No comments:
Post a Comment