Tanzania na Kenya kuandaa pamoja kongamano la Bonde la Mto Mara - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 14, 2025

Tanzania na Kenya kuandaa pamoja kongamano la Bonde la Mto Mara


Katibu Mkuu wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ametoa wito kwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kilichoko Wilayani Butiama Mkoani Mara na Chuo Kikuu cha Masai-Mara kilichoko nchini Kenya kuandaa kwa pamoja chini ya Uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria Kongamano la Kisayansi la 15 la Bonde la Mto Mara kwa mwaka 2026.

Wito huo ameutoa leo wakati akifungua Kongamano la 14 la Kisayansi la Bonde la Mto Mara katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia mjini Butiama mkoani Mara.

Kongamano hilo limehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Kenya na Tanzania wakiwemo wawakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Maasai Mara cha Kenya pamoja na Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia

Amesisitiza kuwa mahusiano ya Tanzania na Kenya yamekuwa ya muda mrefu na yamezalisha matunda mbalimbali ikiwemo ulinzi wa mto Mara ambao unaanzia milima ya Mau nchini Kenya hadi ziwa Victoria nchini Tanzania 

Amesema jitihada za pamoja zitawezesha kupatikana wafadhili wa kudumu ambao watasaidia kuendeleza jitihada za viongozi wa nchi mbili za Kenya na Tanzania katika kupata suluhisho la changamoto zinazolikumba bonde la Mto Mara

Mhandisi Mwajuma amesema hana mashaka na utendaji mzuri wa Chuo cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere na ametoa wito maalum kwa Chuo hicho kuchangamkia fursa aliyoitambulisha kwa jina la Mara Valley Development Project ambayo inahusisha ujenzi wa Bwawa la Borenga katika vijiji vya Borenga na Mrito kwa ajili ya kilimo na matumizi mengine. 

“Mradi huo umeandaliwa, unahitaji fedha za kuendeleza. Kwa kuwa hiki ni Chuo cha Kilimo na mradi uko hapa ndani ya mkoa, pokeeni fursa hiyo.” Mhandisi Mwajuma amesema. 

Aidha katika kongamano la 14 Mhandisi Mwajuma amewataka Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, Chuo Kikuu cha Masai-Mara na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria chini ya uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria wahakikishe wanaandaa andiko la Mradi wa Kuhifadhi Bonde la Mto Mara. 

Maadhimisho ya 14 ya Bonde la Mto Mara kwa mwaka 2025 yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo Hifadhi Mto mara, Tunza Uhai

No comments:

Post a Comment