
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), iko kwenye mchakati wa kuanzisha Vituo vidogo vya Utafiti wa mbegu za viazi mviringo pamoja na tufaa katika Vijiji vya Ibaga na Iniho vilivyoko katika Wilaya ya Makete Mkoani Njombe kutokana na umuhimu na uhitaji wa mbegu hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt, Thomas Bwana akiwa ameongozana na wataalam mbalimbali kutoka TARI, mnamo Septemba 10, 2025, wametembelea na kukagua maeneo katika vijiji vya Ibaga na Iniho Mkoani Njombe na kuridhia kuanzisha vituo hivyo vidogo vya utafiti wa mbegu za mazao hayo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya ukaguzi wa maeneo hayo, Dkt, Bwana amesema katika Kijiji cha Ibaga kutaanzishwa kituo kidogo cha Utafiti wa mbegu za viazi mviringo na katika kijiji cha Iniho kutaanzishwa kituo kidogo cha Utafiti wa mbegu za Tufaa.
"Hakuna haja ya kuendelea kuchelewa kuanzishwa kwa vituo hivyo vidogo vya utafiti wa mbegu za mazao hayo kutokana na uhitaji mkubwa wa mbegu hizo ili kuwasaidia wakulima wa mazao hayo kupata mbegu bora zenye tija," alisema
Aliongeza: “Sisi TARI, hatutaki kumcheleweshea mkulima mafanikio, mkulima hatakiwi kuwa na sababu ya kujitetea kuwa amekosa mbegu bora za kilimo, au wataalam wa kilimo wakati TARI tupo,"
" Jukumu letu ni kutatua changamoto za wakulima katika uzalishaji, tunatakiwa kuwepo nyakati zote ili kuwasaidia wakulima ” alisema Dkt. Bwana.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Jerry Daimon Mwaga, amesema kuwa lengo la halmashauri ni kuhakikisha kuwa wanatafuta fursa mbalimbali za masoko pamoja na kuboresha kilimo kwa wakulima ili waweze kukua kiuchumi.
Ameongeza kuwa Halmashauri ya Makete imedhamiria kuhakikisha inaboresha mazingira ya uzalishaji wa mazao ndani ya wilaya ya Makete, na kutafuta fursa mbalimbali za uboreshaji wa kilimo kutokana na mchango mkubwa katika uchumi wa Makete.
Kuhusu TARI, Mwaga amesema anaamini TAASISI hiyo itachangia kwa sehemu kubwa katika utafiti wa Mbegu bora za viazi Mviringo pamoja na Tufaa na kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa mbegu bora za mazao hayo katika Halmashauri hiyo.
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ndg. Evance Mdee, amesema kuwa zaidi ya ekari 600 zimetengwa kwa ajili ya Uwekezaji wa Utafiti na uzalishaji wa Mbegu bora za Kilimo cha viazi mviringo katika vijiji vya Malembuli na Ibaga na ekari 325 zimetengwa kwa ajili ya utafiti na uzalishaji wa mbegu za tufaa ikiwa ni pamoja na mpango wa uwekaji wa mifumo ya umwagiliaji ili utafiti na uzalishaji uweze kufanyika katika misimu yote ya kilimo.




No comments:
Post a Comment