Chama Cha Mapinduzi CCM kimesema kila ambacho wanakifanya nchini Tanzania ikiwemo uwekezaji mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanywa na serikali yake ni sehemu jitihada zake na matamanio yake katika kujali utu wa kila Mtanzania.
Kauli hiyo imesemwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa awamu ya sita na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, wakati wa Mkutano wake wa Kampeni leo Septemba 09, 2025 Mjini Singida, akiutaka Mkoa huo pia kama Mkoa wa baraka kwa Watumishi wa umma na wa sekta binafsi nchini kutokana na mabadiliko ya maslahi aliyotangaza wakati wa sherehe za Wafanyakazi Mei Mosi, 2024.
"Chama Cha Mapinduzi kinaweka ilani, kuweka uwekezaji, kutumia fedha nyingi kama zilivyotajwa ili kujali na kuinua utu wa mtu. Tunataka kila Mtanzania tujali utu wake, tujali afya yake, tujali elimu yake, tujali usalama wake, tujali kila kitu kinachomgusa mtanzania hata uchumi na ustawi wake, kwahiyo yote tunayoyafanya ni kujali utu wa Mtanzania, tunaowamba tupeni ridhaa twende tukafanye makubwa zaidi yanayomjali Mtanzania." Amesisitiza Dkt. Samia.
Dkt. Samia pia amewashukuru Machifu na viongozi wa kimila mkoani Singida kwa zawadi ya mafuta ya alizeti waliyompatia, akisema mafuta hayo yatatumika kwa Maafisa na Viongozi anaoambatana nao kwenye kampeni hizo za kuelekea uchaguzi Mkuu wa baadae mwezi Oktoba.
No comments:
Post a Comment