
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema kuwa mgombe Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiwezesha Kata ya Uyovu kimaendeleo hivyo wananchi hao hawana budi kumpigia kura nyingi Oktoba 29 mwaka huu.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 17, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Uyovu wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“ Hakuna siku ambayo nilimuomba maendeleo Dkt. Samia kwa ajili ya watu wa Uyovu na Geita akatunyima, ametupa fedha za ujenzi wa barabara nyingi ikiwemo ya kutoka Ushirombo hadi Katoro hata juzi tulimuomba barabara ya Geita kwenda Nzela hadi Sengerema kwa kiwango cha lami yote haya atatusaidia huyu ni mama ni msikivu,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Dkt. Samia chini ya CCM katika Kata ya Uyovu wamefanikiwa kujenga shule za msingi 11 na shule binafsi moja kutoka shule tatu, shule za sekondari saba na shule moja ya kidato cha tano na sita.
Pia, amesema katika Wilaya ya Bukombe kuna shule mbili za watoto wenye mahitaji maalum ambapo moja ipo Uyovu na nyingine Ushirombo.
Ametaja miradi mingine ya maendeleo iliyotekelezwa katika Kata hiyo ni pamoja na kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami, hospitali, zahanati pamoja na mradi wa maji uliogharimu sh. bilioni 1.1.
Kuhusu kuifanya Uyovu kuwa kitovu cha biashara amesema kuwa CCM itaongeza msukumo kwa kusogeza miundombinu ya kuiwezesha Kata hiyo kuvutia shughuli za biashara kwa wingi.
Vilevile, CCM itatoa mkopo wa sh. bilioni 200 kwa vijana na wanawake ili kuwawezesha wafanyabiashara ikiwemo wa Uyovu.
Pamoja na hayo amesema miaka mitano ijayo Uyovu itakuwa na maendeleo zaidi hivyo wananchi 35,000 wa Kata hiyo waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze kwa wingi Oktoba 29 na kumchagua Dkt. Samia.
Amesisitiza “ Sasa maendeleo haya hayajatokea kwa bahati mbaya kama kuna mtu anatupenda ni Dkt. Samia, Uyovu ni jeshi kubwa mkapige kura nyingi ili tuwe na sababu ya kuwaletea maendeleo,”
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma amesema kuwa wananchi wa Uyovu wana ajenda moja ya maendeleo na hivyo amewaomba wananchi hao kuwaamini na kuwapigia kura wagombea wa CCM.
“ Ninyi ni mashahidi kwa miaka kumi ya uongozi wa Biteko hapa Bukombe tumepiga hatua katika elimu na maeneo mengine. Sasa tunasimama hapa tukiwa na shule za msingi 11 katika Kata yetu na nyingine zikiendelea kujengwa ili kusaidia watoto wetu,” amesema Kagoma
Amewaeleza kuwa sababu ya kumchagua Dkt. Biteko ni kwa kuwa wanahitaji kupiga hatua ya maendeleo zaidi katika maeneo mengine ikiwemo afya.




No comments:
Post a Comment