VIJANA NA WANAWAKE KUCHOCHEA USHINDI WA KISHINDO KWA DKT. SAMIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 10, 2025

VIJANA NA WANAWAKE KUCHOCHEA USHINDI WA KISHINDO KWA DKT. SAMIA



Mratibu wa Kampeni za Kitaifa za Chama Cha Mapinduzi CCM na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama hicho tawala Dkt. Bashiru Ali, amesema Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama hicho ataibuka na ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kutokana na wingi mkubwa wa Vijana na wanawake wanaojitokeza kwenye kampeni za Chama hicho.

Bashiru ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 10, 2025 Nzega Mjini Mkoani Tabora kwenye siku ya kwanza ya kampeni za Dkt. Samia Mkoani humo, akisema katika kipindi cha miaka minne ya Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa, Jumuiya za Chama hicho zimeimarika pakubwa, suala ambalo amesema Jumuiya hizo sio kama zilivyokuwa wakati wa Uongozi wake.

"Tumekuwa na kiwango cha chini sana cha wapigakura, miaka mingi wala sio mwaka huu wala 2020 lakini sasa hivi nina uhakika kwa kuwa akinamama wamehamasika na Vijana wamehamasika nadhani kuna uwezekano mkubwa wa kufikia idadi ya zaidi ya asilimia 90 ya wapigakura mwaka huu. Kwa takwimu za nchi yetu, Vijana ndio wengi na akinamama ndio wengi nchi hii lakini la pili linalosababisha watu kutotoka kupiga kura ni mikakati ya kutisha watu kwa maneno au vitendo, nina hakika serikali ya CCM ina wajibu wa kulinda kila aliyejiandikisha kwenda kupiga kura kwa amani na kusherehekea ushindi kwa amani na kwa maandalizi.

Mwitikio na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kwa mvuto wa mgombea wetu tutashinda kwa kura nyingi na waliojiandikisha wengi watapigakura." Amesema Dkt. Bashiru.

Dkt. Bashiru ameongeza kusema kuwa "Kampeni ni fursa muhimu sana hasa katika nchi ya amani kama Tanzania, ni fursa ya kuibua hisia za watu kuhusu hali ya maisha yao, hali ya uendeshaji wa nchi yao. Ni fursa ya kuwajengea wananchi matumaini na matarajio, ni fursa pia kwa baadhi ya wengine kuwa na wasiwasi lakini katika nchi ambayo haina misingi imara hii ni fursa ya vurugu na mipasuko ya kijamii. Mimi sina mashaka na nchi yetu misingi yake, nafasi ya uchaguzi kutuvuruga na kutupasua bado haijawepo na kwasababu bado haijawepo tusibweteke."

Kesho Dkt. Samia atakuwa na mikutano ya hadhara Uyui, Urambo na Kaliua kabla ya Septemba 12, 2025 kuhitimisha mikutano yake Mkoani humo kwenye Viwanja vya Nanenane Manispaa ya Tabora.




No comments:

Post a Comment