
Na Mwandishi Wetu, Bukoba
Wananchi ambao wanapitiwa na miradi ya Barabara wametakiwa kulinda na kuhifadhi miradi ya Barabara na kuachana na dhana ya kutupa uchafu katika mitaro ya maji inayokuwa imetengenezwa na kusababisha uchafuzi wa Barabara.
Wito huo umetolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ndugu Ismail Ussi wakati akiweka jiwe la Msingi katika barabara ya Ihungo yenye urefu wa Km. 1.25 yenye thamani ya shilingi Milioni 506.4 ambayo inaunganisha kata za Kashai na Shambya kwa kiwango cha lami inayotekelezwa na TARURA.
"Kumekuwa na tabia ya uchafuzi wa mazingira kwa barabara zinazopita karibu na makazi yenu,mtu anakusaya taka anatupa katika mitaro anasema mvua ikinyesha itasafirisha uchafu hii haikubariki na imeharibu barabara nyingi , tutunze na kuthamini Miradi inayoletwa kwa sababu inatumia pesa nyingi sana "Amesema Ussi
Aidha, ameipongeza TARURA kwa kuendelea kung’arisha mji wa Bukoba hasa mitaa ya pembezoni kwa kuwawekea lami na taa za barabarani jambo ambalo linakuza uchumi wao kwa kufanya biashara usiku na mchana.
Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Bukoba Mhandisi Emmanuel Yohana amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu tatu na lengo kuu ni kuendelea kuweka lami katika mitaa na kupendezesha mji wa Bukoba
Amesema mradi huu umefika asilimia 40 na ulianza kutekelezwa Septemba mwaka 2024 na utakamilika Novemba 2025 ili wananchi wa Kata ya kashai na Nshambya wanaunganishwa na barabara hiyo waendelee kuitumia barabara kwa urahisi pamoja na wananchi kufanya biashara nyakati za usiku baada ya kuwekewa taa.





No comments:
Post a Comment