
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani anayoinadi ya 2025/30 ameahidi kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani utakaojengwa katika msingi wa kuongeza thamani rasilimali zinazozalishwa nchini.
Dkt. Samia ambaye amehitimisha Kampeni zake kwenye Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, akitarajiwa kuanza Kampeni Kanda ya Ziwa, akianzia na Mwanza Oktoba 07, 2025, ameeleza kuwa lengo ni kuimarisha ukuaji jumuishi wa uchumi na Kukuza uchumi kwa wastani kwa mwaka kufikia asilimia 7 kutoka asilimis 5.6 iliyopo hivi sasa.
Ameahidi pia kutekeleza mpango wake wa kuanzisha mfuko maalum wa kuwezesha upatikanaji wa mitaji, hususani kwa wajasiriamali wa biashara ndogo, za kati na kampuni changa, mfuko utakaoanza na Bilioni 200 ndani ya siku zake 100 za awali madarakani, kiwango ambacho kitaongezeka kadiri ya marejesho ya fedha hizo itakavyokuwa.
"Tutaongeza pia miundombinu ya umwagiliaji itakayoongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji, kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora na kwa bei nafuu na kuendelea kutoa ruzuku za mbolea na pembejeo, kuanzisha vituo vya ukodishaji zana za kilimo, tukitarajia pia kutoa matrekta 10,000 kwa mkopo." Amesisitiza Dkt. Samia katika Mikutano yake.
Dkt. Samia pia ameahidi kuwezesha upatikanaji wa mitaji, mikopo na vifaa kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji, Vyama vya ushirika na wawekezaji ikiwa ni sambamba na kuendeleza Viwanda saba vya National steel, Nachingwea Cashew nuts, Mafuta Ilulu, TPL Mbeya, TPL Shinyanga, Sawmill pamoja na Kiwanda cha Mwanza Tannery.
Katika sekta ya Uzalishaji kuelekea mwaka 2030, Dkt. Samia ameahidi kuongeza sekta ya uzalishaji Viwandani kufikia asilimia 9 kwa mwaka 2030, kufanya tafiti zaidi za maeneo yenye madini na kuongeza eneo lililopimwa ili kukuza sekta hiyo kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 50 mwaka 2030, akiahidi pia kuifanya Tanzania kuwa kituo cha uuzaji wa madini katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kati pamoja na kuimarisha masoko ya madini na vito ikiwemo Tanzanite kwa kujenga Jengo la Tanzanite Exchange Centre katika eneo la Mirerani, Simanjiro.
No comments:
Post a Comment