
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 08, 2025 amempokea na Kumkaribisha kwenye Chama hicho aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza Bw. Boniface Paul Mkobe Nzagamba.
Dkt. Samia amempokea Mwanasiasa huyo aliyewahi pia kuwa Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema Mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha miaka kumi, akisisitiza kuwa kupokelewa kwa Bw. Nzagamba ni ishara ya siasa safi za Chama Cha Mapinduzi tofauti na "kule alipotoka, Chama cha wanaharakati."
"Na hii ndio faida ya siasa safi, mkiwa na siasa safi wale wanasiasa wa kweli huwafuata wenye siasa zilipo lakini wale wanaharakati hubakia na Chama chao cha wanaharakati. Natambua Chama kilekile anachotoka boniface, wanasiasa wa kweli wameenda kujiunga na vyama vingine kufuata siasa za kweli." Ameeleza Dkt. Samia.
Awali Bw. Nzagamba ameeleza furaha yake ya kujiunga ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM pamoja na kupewa fursa ya kusalimia mbele ya umati mkubwa wa wananchi, jambo ambalo halikuwahi kutokea kwenye maisha yake, akisema ameamua kujitokeza hadharani kutokana na kutokubaliana na baadhi ya hoja na maelekezo ya Uongozi wa Chama chake cha zamani, kinachohamasisha maandamano siku ya Oktoba 29, 2025, siku ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania.




No comments:
Post a Comment