
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Ijumaa Oktoba 24, 2025 anatarajiwa kuomba kura kwa wananchi na kufunga Kampeni zake Visiwani Zanzibar kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Unguja, tayari kwa uchaguzi Mkuu wa Jumatano Ijayo ya Oktoba 29, 2025.
Dkt. Samia anafanya Kampeni zake.Unguja akitokea kwenye Kampeni zake Mkoani Dar Es Salaam ambapo katika maelekezo ya Chama Chake kupitia Ilani anayoinadi Dkt. Samia, Chama kimeelekeza kuendelea kuwaunganisha Wazanzibar, kudumisha umoja, amani, utulivu, ushirikiano, maridhiano na uvumilivu sambamba na kuendelea kuwashirikisha wananchi katika kujenga uchumi imara ambao utazingatia usawa na kunufaisha maeneo yote Visiwani Zanzibar.
Chama pia kimemuelekeza Dkt. Samia kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa Vijana kwa kuzalisha angalau ajira 350,000 kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi, kufanya mageuzi katika sekta za kilimo kwa kuongeza uzalishaji wa ndani na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa kuanzisha hifadhi ya Taifa ya chakula na kuendelea kuimarisha miundombinu wezeshi ya kiuchumi ikiwemo bandari, barabara na viwanja vya ndege ili kusisimua shughuli za kiuchumi na Kijamii.
Aidha Dkt. Samia pia ameelekezwa kusimamia uimarishaji wa sekta ya mafuta na gesi kwa lengo la kuendeleza jitihada za kuongeza vyanzo vya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kwa kuendeleza utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, kutangaza na kugawa vitalu vipya vya uwekezaji wa mafuta na gesi asilia na kujenga kituo cha kudumu cha kuhifadhi taarifa na sampuli za mafuta na gesi asilia.
CCM pia imeahidi kuendelea na ujenzi wa bandari jumuishi katika maeneo ya Mangapwani inayojumuisha bandari ya mizigo, uhifadhi wa makontena na mizigo, maegesho ya meli, maeneo maalumu ya kuhifadhi mafuta na gesi, kujenga bandari za kisasa za abiria za Mpigaduri na Kizimkazi kwa Unguja na bandari za Shumba na Wete, Pemba.
Katika Hatua nyingine Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka leo Oktoba 24, 2025 ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya mapumziko ili kutoa fursa kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wenye sifa stahiki kwenda kupiga kura Hapo Oktoba 29 ili kuwachagua Wabunge, Madiwani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:
Post a Comment