
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambaye pia ni Mwenyekiti wq Chama Cha Mapinduzi Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Jioni Oktoba 13, 2025 amefika Chato Mkoani Geita nyumbani kwa familia na sehemu alipozikwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na kuweka shada la maua pamoja na kumuombea dua ya kuendelea kupumzika kwa amani.
Dkt. Samia amefika kwenye Makaburi hayo ya familia Rubambangwe Chato akiambatana na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Balozi Dkt. Asha- rose Migiro na baadhi ya wanafamilia mara baada ya kuhitimisha Mkutano wake wa kampeni Katika Wilaya hiyo ya Chato Mkoani Geita.
Hayati Dkt. John Magufuli alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Tano wa Tanzania, akiongoza serikali kwa miaka yote mitano ya awamu ya kwanza na takribani mwaka mmoja katika awamu ya pili akiwa na Makamu wake kipindi hicho Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mpaka pale mauti ilipomfika Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar Es Salaam alipokuwa akitibiwa, akiweka rekodi enzi za uhai wake kama Rais wa kwanza wa Tanzania kumuamini na kumteua Makamu wa Rais mwanamke katika Historia ya Tanzania.






No comments:
Post a Comment