
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 anaendelea na Kampeni za uchaguzi Mkuu Bukoba Mjini Mkoani Kagera, akitarajiwa kunadi Ilani ya Chama chake, kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita pamoja na kuomba kura katika Viwanja vya Kaitaba Bukoba Mjini.
Jana Jumatano Dkt. Samia alianza kampeni zake Mkoani humo, akifanya Mikutano Muleba, Kyaka na Kayanga, akiahidi ujenzi wa uwanja wa ndege Missenyi, ugawaji wa mbegu za parachichi na kahawa, utoaji wa ruzuku za mbolea na pembejeo za kilimo, uwezeshaji katika sekta ya uvuvi, usimamizi wa kilimo cha Vanila sambamba na uendelevu wa utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo miundombinu ya elimu, afya na usambazaji wa umeme.
Katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM anayoinadi Dkt. Samia kwa Bukoba Mjini ndani ya Miaka mitano ijayo imeahidi Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, Vituo vya afya na Zahanati katika Kata na Vijiji vyote, Ukamilishaji wa kituo cha afya Kagondo, Ujenzi wa shule moja ya Kata, madarasa 131, Ukarabati wa shule kongwe 4, madarasa, nyumba za waalimu na mabweni 2 ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule za msingi ndani ya Manispaa hiyo.
Aidha CCM imeahidi kutekeleza Ujenzi wa madarasa 28, maabara 11, maktaba na nyumba 4 za waalimu katika shule za sekondari, Ujenzi wa masoko 5 ya Machinjioni, Kagondo, Rwamishenye, Kashai na Kyabitembe sambamba na ujenzi wa kitega uchumi eneo la Mayunga.
Ndani ya miaka mitano ijayo CCM pia imeahidi Kuimarisha miundombinu ya bandari ya Kemondo pamoja na kuboresha barabara za Manispaa ya Bukoba.
Kwa miaka minne ya serikali ya awamu ya sita pamoja na masuala mengine, Serikali kwa Wilaya ya Bukoba ilifanikisha Ujenzi wa Hospitali mbili za Bukoba DC na Manispaa, ujenzi na ukarabati wa shule za msingi na sekondari, kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama Vijijini kutoka asilimia 76 hadi 83, Ujenzi wa bandari ya Bukoba, kuendeleza ujenzi wa Kituo kikuu cha mabasi ya Bukoba, ujenzi wa barabara ya njia nne Bukoba Mjini, kuendelea na ujenzi wa soko kuu la Bukoba.
No comments:
Post a Comment