
Zikiwa zimesalia siku kumi pekee ili Watanzania wenye sifa kuweza kuteremka kwenye Vituo vya kupigia kura, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa leo Oktoba 19, 2025 kuwa na Mkutano mkubwa wa Kampeni Sumbawanga mjini.
Dkt. Samia anaingia Sumbawanga Mjini akitokea kwenye Wilaya za Mlele na Nkasi, akiomba kura kwa wananchi kwa ujasiri mkubwa kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi chake cha miaka minne madarakani ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Hospitali 4 za Halmshauri za Wilaya za Sumbawanga, Nkasi, Kalambo pamoja na Hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga.
Wamenunua pia magari nane ya kubebea wagonjwa, kukamilisha majengo 3 ya huduma za dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo na Nkasi, Kuongeza idadi ya Zahanati kutoka 164 hadi 198, kuongeza vituo vya afya kutoka 13 hadi 30, kuongeza upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 76 hadi 89 na kupunguza vifo vya akinamama wajawazito kutoka 128 kwa vizazi hai 100,000 hadi vifo 60 kwa vizazi hai 100,000 na Vifo vya watoto wachanga vipengua kutoka 11 kwa vizazi hai 1, 000 hadi vifo saba kwa kila vizazi hai 1,000.
Kwa upande wa elimu, Jumla ya shilingi 9, 980,000,000 zimetolewa kugharamia sera ya elimu bure kutoka 3, 640,000,000, kuongezeka kwa idadi ya shule za msingi kutoka 387 hadi 420 huku Sekondari zikiongezeka kutoka 97 hadi 120, kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya chuo cha ualimu Sumbawanga pamoja na ujenzi wa Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Kampasi ya Rukwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwa gharama ya Bilioni 14.8.
Serikali ya awamu ya sita imekarabati pia uwanja wa ndege Sumbawanga, kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara zenye jumla ya Kilomita 13.03 kwa kiwango cha lami Manispaa ya Sumbawanga, kukamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 3 katika Wilaya ya Sumbawanga katika barabara ya Ntendo- Muze- Kilyamatundu, pamoja na ukamilishaji wa upanuzi wa gati za bandari ya Kasanga na Kabwe pamoja na usimikaji wa taa 197 za barabarani zilizoimarisha biashara na usalama nyakati za usiku Mjini Sumbawanga.
Katika upande wa miradi ya Kimkakati serikali ya Dkt. Samia imeanza ujenzi wa miundombinu ya soko katika Mji wa Matai pamoja na kujenga soko la kisasa la mazao lililopo katika eneo la Kanondo Manispaa ya Sumbawanga.
Kuelekea mwaka 2030 ikiwa Dkt. Samia atapewa ridhaa ya kuongoza serikali,pamoja na mambo mengine kwa Wilaya ya Sumbawanga ameahidi upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege Sumbawanga, Ujenzi wa stendi ya mabasi Laela, Ujenzi wa skimu 33 za Umwagiliaji kwa Wilaya zote za Mkoa huo, ujenzi wa Bwawa la Mwambazi, Ujenzi wa soko la wakulima Ndelema pamoja na ukamilishaji wa mabweni kwa shule za msingi za mahitaji maalumu Kizwite na Malangali pamoja na ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje kwenye Zahanati 22 za Sumbawanga.
No comments:
Post a Comment